Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, imekamilisha awamu ya kwanza na muhimu zaidi ya maandalizi yake kuelekea Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), huku benchi la ufundi likithibitisha kuwa wachezaji wote wako fiti kimwili na tayari kwa awamu inayofuata ya mbinu na ufundi.
Akizungumza kutoka kwenye kambi ya timu hiyo iliyopo mji wa Ismailia, nchini Misri, Kocha Msaidizi Juma Mgunda, alisema program yao ya mazoezi ya siku 10 imefanikiwa kwa kiasi kikubwa, hasa katika eneo la kuwajenga wachezaji kuwa na utimamu wa mwili wa kushindana.
"Tunashukuru Mungu, kile tulichokipanga kinakwenda vizuri. Kazi kubwa ya kujenga utimamu wa mwili imekamilika na wachezaji wako fiti. Sasa tunaingia kwenye hatua ya pili, ambayo ni ya kiufundi na mbinu, na tutamalizia na maandalizi ya kisaikolojia," alisema Mgunda.
Mgunda aliwatoa hofu Watanzania, akisema kuwa morali ya wachezaji kambini ipo juu sana. Alisema wachezaji wanatambua kuwa wana deni kubwa kwa taifa, hasa kwa kuwa mashindano hayo yanafanyika nyumbani na mechi zao zote za kundi zitachezwa Dar es Salaam.
"Wachezaji wameahidi kupambana. Wanajua fika umuhimu wa kufanya vizuri mbele ya mashabiki wetu. Kazi yetu sisi makocha ni kuwaandaa, lakini wao ndio watakaoenda kutuwakilisha uwanjani," alisisitiza.
Taifa Stars, inayoundwa na wachezaji wanaocheza ligi za ndani, itafungua dimba la michuano hiyo Agosti 2, mwaka huu, kwa kupambana na Burkina Faso katika Uwanja wa Benjamin Mkapa. Ipo Kundi B pamoja na timu za Burkina Faso, Afrika ya Kati, Madagascar, na Mauritania.
Michuano ya CHAN mwaka huu inafanyika kwa ushirikiano wa nchi tatu za Afrika Mashariki: Tanzania, Kenya, na Uganda.