Siku chache tu baada ya droo ya Ligi ya Mabingwa Afrika kuipanga Simba SC dhidi ya Gaborone United ya Botswana, Kocha Mkuu wa Wekundu wa Msimbazi, Fadlu Davids, amewasha moto akitangaza kuwa tayari ameanza maandalizi ya kiintelijensia kwa kuwatuma wasaidizi wake kuwapeleleza wapinzani wao hao. Akizungumza jana kutoka kambini nchini Misri, kocha huyo raia wa Afrika Kusini ameweka wazi kuwa hana mzaha na anataka kujua kila kitu kuhusu Gaborone United kabla ya pambano lao la hatua ya awali mwezi Septemba.
Fadlu Davids alisema anaheshimu sana soka la Botswana, akitoa mfano wa jinsi walivyopata wakati mgumu walipokutana na Jwaneng Galaxy hapo awali. Alieleza kuwa timu za Botswana zina wachezaji wenye kasi na wanaopenda kukimbia muda wote, jambo linalohitaji maandalizi ya hali ya juu. "Watu wangu wa uchambuzi wameshaanza kazi mara moja kuichunguza timu hiyo ili tujue ina nguvu wapi na udhaifu wake ni upi," alisema Fadlu, akionyesha umakini wake katika maandalizi.
Pamoja na kuwaheshimu wapinzani wao, kocha huyo alionyesha kujiamini kutokana na ubora wa kikosi chake, ambacho kina mchanganyiko mzuri wa wachezaji wenye uzoefu na chipukizi wenye njaa ya mafanikio. Alisema maandalizi wanayoyafanya nchini Misri ni ya kiwango cha juu na yanalenga kuwafanya wawe tayari kwa vita yoyote.
Katika hatua nyingine, Fadlu Davids ametoa tamko zito kuhusu uwanja wa nyumbani wa timu hiyo. Alisisitiza kuwa safari hii, Simba inataka kucheza mechi zake zote za nyumbani katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, na hawatakubali kupelekwa tena Zanzibar kama ilivyotokea msimu uliopita kwenye Kombe la Shirikisho. "Nafikiri safari hii hawatotupeleka tena Zanzibar. Hatuhitaji hilo, tunataka tucheze Benjamin Mkapa kwa sababu kila kisichowezekana pale, kinawezekana," alisisitiza kocha huyo.
Wakati huo huo, kikosi cha Simba kimemaliza awamu ya kwanza ya mazoezi ya kujiweka fiti kimwili na sasa kimeingia katika awamu ya pili ya mazoezi ya kiufundi na mbinu uwanjani. Hii ina maana kuwa kocha sasa anaanza kutengeneza mifumo na muunganiko wa timu yake kuelekea msimu mpya wa mashindano.