Kocha Mkuu wa Simba SC, Fadlu Davids, ameweka wazi kuwa licha ya kuridhishwa na wachezaji wapya waliosajiliwa, bado anaona pengo la mshambuliaji mmoja hatari anayeweza kubeba timu na kuamua matokeo ya mechi ngumu. Kauli hiyo ameitoa akiwa nchini Misri, ambako kikosi cha Wekundu wa Msimbazi kilikuwa kimeweka kambi ya maandalizi ya msimu mpya.
Mkufunzi huyo raia wa Afrika Kusini alisisitiza kuwa ili kufikia malengo makubwa ya msimu ujao, ambayo ni pamoja na kufanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na kutetea heshima mbele ya watani wao Yanga, wanahitaji straika wa daraja la juu. Alikumbushia baadhi ya mechi muhimu za msimu uliopita ambapo walikosa mchezaji wa aina hiyo.
"Mnakumbuka mechi kama ile ya fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya RS Berkane, au hata kwenye michezo yetu dhidi ya Yanga, tulitamani kuwa na mchezaji ambaye anaweza kuibuka na kufanya kitu cha tofauti wakati mambo yanapokuwa magumu," alisema Fadlu. Aliongeza kuwa anahitaji mchezaji mwenye uwezo wa kufanya maamuzi binafsi yatakayoipa timu ushindi.
Kwa mujibu wa Fadlu, suala la kumpata mchezaji huyo sasa liko mikononi mwa viongozi wa juu wa klabu. Alimwelekezea moja kwa moja ombi lake kwa Rais wa Heshima, Mohamed Dewji, na uongozi wa wadhamini chini ya Mkurugenzi Joseph Rwegasira, akiamini kuwa wanaweza kukamilisha usajili huo kabla ya dirisha kufungwa.
Wakati akitoa ombi hilo, timu yake ilikuwa imetoka kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Wadi Degla SC ya Misri, magoli yakifungwa na Elie Mpanzu pamoja na Kibu Denis. Hata hivyo, alidokeza kuwa wangeweza kushinda kwa idadi kubwa zaidi ya magoli endapo wachezaji wake wangekuwa na umakini wa kutosha.
Simba inatarajiwa kurejea nchini leo baada ya kambi ya takriban mwezi mmoja nchini Misri, ambapo walicheza mechi nne za kirafiki, wakishinda tatu na kupoteza moja.