Simba Yafunguka Isu ya Bajaber na Kocha Pantev, Mashabiki Watulizwa Moyo

sports | Mon Oct 13 2025


Simba Yafunguka Isu ya Bajaber na Kocha Pantev, Mashabiki Watulizwa Moyo

Hatimaye kile kilichokuwa kikiwasubirisha kwa hamu mashabiki wa klabu ya Simba kimetimia, baada ya uongozi wa timu hiyo kuthibitisha kuwa kiungo mshambuliaji mwenye makeke na mbwembwe nyingi, Mohamed Bajaber, amerejea uwanjani na kuanza mazoezi mepesi. Hii ni habari njema kuelekea mtanange muhimu wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Nsingizini Hotspurs kutoka Eswatini.


Bajaber, raia wa Kenya aliyesajiliwa kutoka klabu ya Police FC, alitua Msimbazi akiwa na majeraha, hali iliyomfanya ashindwe kuonyesha ufundi wake tangu msimu uanze. Kulingana na Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, ilikuwa ni kwa amri ya aliyekuwa kocha Fadlu Davids kwamba mchezaji huyo asajiliwe licha ya hali yake, kutokana na kuvutiwa mno na kipaji chake. "Kocha aliona uwezo wake na akasisitiza tumchukue akapate matibabu hapa. Ingawa alipona mapema, jopo la madaktari lilitushauri asitumike hadi apone kwa asilimia mia moja," alifafanua Ahmed.


Wakati kukiwa na matumaini mapya ya kumwona Bajaber akicheza, upande wa pili kumekuwa na mjadala kuhusu cheo cha kocha mpya, Dimitar Nikolaev Pantev, ambaye amepewa nafasi ya "Meneja Mkuu" badala ya "Kocha Mkuu." Ahmed Ally alituliza mashabiki kwa kueleza kuwa cheo cha Meneja Mkuu kina hadhi na majukumu makubwa zaidi. Alisema, "Meneja Mkuu sio tu anafundisha timu, bali anahusika na mapendekezo ya usajili na maono mapana ya kiufundi. Kila meneja anaweza kuwa kocha, lakini si kila kocha anaweza kuwa meneja."


Hata hivyo, taarifa za ndani zinadokeza kuwa huenda hatua hiyo imechukuliwa ili kukwepa masharti ya leseni kwa makocha kwenye michuano ya kimataifa, ambapo Pantev huenda hangetimiza vigezo vya kuwa Kocha Mkuu.


Licha ya maneno hayo, Simba imesimama kidete kumtetea kocha huyo, ikieleza kuwa sifa zake ni za kipekee. Kilichowavutia zaidi ni rekodi yake ya kubeba ubingwa mara mbili mfululizo katika nchi mbili tofauti; kwanza akiwa na Victoria United ya Cameroon msimu wa 2023/24 na kisha Gaborone United ya Botswana msimu wa 2024/25. "Lakini pia tuliona alivyotufunga akili tulipocheza naye. Aliifanya Gaborone United, timu ndogo, ionekane kama Simba, na sisi tukawa kama wao. Kocha wa aina hii ndiye tunayemhitaji," aliongeza Ahmed.


Simba inatarajiwa kuwakaribisha Nsingizini Hotspurs katika mchezo wa kimataifa ifikapo Oktoba 19, mwaka huu.


The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.