Vita Dhidi ya Bangi Hifadhini: DCEA, TANAPA Zateketeza Ekari 614, Zasambaratisha Kambi 72

politics | Wed Jul 16 2025


Vita Dhidi ya Bangi Hifadhini: DCEA, TANAPA Zateketeza Ekari 614, Zasambaratisha Kambi 72

Katika operesheni kali ya pamoja, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) zimefanikiwa kuteketeza ekari 614 za mashamba haramu ya bangi na kusambaratisha kambi 72 za wakulima zilizokuwa zimejificha katika ushoroba wa Hifadhi za Taifa za Mikumi na Nyerere.


Akizungumza na waandishi wa habari, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, alisema operesheni hiyo imefanikiwa pia kukamata watuhumiwa tisa, pamoja na kilo 3,741.9 za bangi kavu na kilo 1,706 za mbegu za bangi zilizokuwa tayari kwa ajili ya kupandwa.


Kamishna Lyimo alieleza kuwa mafanikio ya operesheni za mara kwa mara yameanza kuonekana, kwani sasa wakulima haramu wa bangi wanalazimika kuhamia maeneo ya mbali zaidi na yaliyojificha, jambo linaloonyesha kuwa shinikizo la vyombo vya dola linafanya kazi.


"Hii ni vita endelevu. Tutaendelea kushirikiana na taasisi zote za ulinzi na usalama kuhakikisha tunatokomeza kilimo hiki haramu. Pia, tunatoa wito kwa wananchi kufanya shughuli halali za kilimo na kuacha kujihusisha na uhalifu huu," alisema Lyimo.


Kwa upande wake, Kamanda Mkuu Msaidizi wa Kikosi cha TANAPA, Moses Oko Onyango, alisema ushiriki wao katika operesheni hiyo ulilenga kulinda maliasili na maeneo ya hifadhi ambayo yalikuwa yameanza kuvamiwa kwa ajili ya kilimo hicho haramu.


"TANAPA inasimamia uhifadhi endelevu. Hatutaruhusu maeneo yetu nyeti ya hifadhi kutumika kwa shughuli haramu. Ushirikiano huu na DCEA ni muhimu na utaendelea kwa kufanya doria za pamoja ili kuhakikisha wahalifu hawarudi tena," alisisitiza Onyango.


Aliongeza kuwa TANAPA, kupitia kitengo chake cha mahusiano na jamii, itashirikiana na DCEA kutoa elimu kwa wananchi na wanafunzi vijijini kuhusu madhara ya dawa za kulevya na umuhimu wa kulinda hifadhi za taifa kwa maendeleo endelevu.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.