Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) nchini Tanzania imetangaza mafanikio makubwa kufuatia kuvunjwa kwa mtandao mzito wa kimataifa wa usafirishaji wa mihadarati. Katika operesheni hiyo, DCEA ilifanikiwa kukamata shehena ya mirungi yenye uzito wa kilo 40.32, ambayo ilikuwa imefungashwa kwa mbinu ya hali ya juu ili kupoteza maboya.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali wa DCEA, Bwana Aretas Lyimo, alieleza kuwa dawa hizo haramu zilikuwa zimefungwa ndani ya paketi 80. Ili kufanikiwa kuzivusha kwenye vituo vya ukaguzi, wafanyabiashara hao walibandika maandishi ya "dry basil leaves" (majani makavu ya mrehani), ili kuonyesha kwamba mzigo huo ulikuwa ni viungo halali vya chakula.
Bwana Lyimo alifafanua kuwa shehena hiyo ilikuwa imeandaliwa kwa ajili ya kusafirishwa kwenda nchi za Canada na Italia. Usafirishaji huo ulipangwa kufanywa kupitia kampuni binafsi za usafirishaji mizigo zilizopo hapa nchini. Kufuatia tukio hilo, tayarI watuhumiwa wawili wamekamatwa na wanashikiliwa kwa uchunguzi zaidi. Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Yusuph Kibaha, mwenye umri wa miaka 35, na Mohamed Ramadhan, mwenye umri wa miaka 41.
Uchunguzi wa awali wa mamlaka hiyo umebaini kuwa mtandao huo umekuwa ukitumia madereva wa bodaboda na hata kuwa na ushirikiano na baadhi ya mawakala wa kampuni za usafirishaji ili kufanikisha uhalifu wao. "Uchunguzi wetu umebaini dawa hizi ziliingizwa nchini kwa njia za kificho kutoka nchi jirani na kuandaliwa kwa ufanisi mkubwa ili zisibainike," alisema Lyimo. Aliongeza kuwa mawakala hao walitumia mbinu za kibiashara kuficha nyendo zao haramu.
Kutokana na mbinu hiyo, Kamishna Lyimo alitoa onyo kali kwa kampuni za usafirishaji mizigo pamoja na waendesha bodaboda kuwa makini na mizigo wanayopokea kutoka kwa wateja. "Madereva wa bodaboda wasiruhusu majina yao kuandikwa kwenye vifurushi wasivyovijua vilivyomo ndani. Na kampuni za usafirishaji ziwe na utaratibu madhubuti wa kuthibitisha taarifa za wahusika, ikiwezekana kuambatanisha na kuhifadhi nakala za vitambulisho vyao," alisisitiza Kamishna.
Katika tukio jingine tofauti, DCEA imefanikiwa kuwanasa vijana wanne katika eneo la Mlalakuwa, Wilaya ya Kinondoni. Vijana hao walikuwa wakijihusisha na utengenezaji na usambazaji wa biskuti zilizochanganywa na bangi, zilizolenga sherehe za wanafunzi wa vyuo vikuu.
Waliokamatwa katika tukio hilo ni Bright Malisa (26), Humphrey Safari (26), Novatus Kileo (26), na Chriss Mandoza (26). Walikutwa na jumla ya biskuti 140 zilizothibitishwa kuwa na bangi, pamoja na puli nane na paketi tisa za bangi zenye uzito wa kilo 2.858.
"Tunaomba wazazi wafuatilie kwa karibu mienendo ya watoto wao walioko vyuoni. Hawa vijana wanatengeneza biskuti hizi zenye bangi kwa ajili ya sherehe za kuzaliwa na hafla mbalimbali za vyuoni, jambo ambalo ni hatari kubwa kwa afya na mustakabali wa elimu yao," alionya Bwana Lyimo.
Akitoa muhtasari wa operesheni za kitaifa, Kamishna Lyimo alisema DCEA kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama imefanya misako katika mikoa 11. Mikoa hiyo ni pamoja na Morogoro, Simiyu, Arusha, Kilimanjaro, Mwanza, Tanga, Pwani, Shinyanga, Ruvuma, Tabora, na Mtwara. Katika misako hiyo, jumla ya kilo 9,164.92 za bangi, kilo 1,555.46 za mirungi, gramu 367 za skanka, na gramu 7.498 za heroin zilikamatwa.
Aidha, kama sehemu ya mkakati wa kudhibiti uzalishaji, jumla ya ekari 11.5 za mashamba ya bangi ziligunduliwa na kuteketezwa katika mikoa hiyo kupitia operesheni za kiintelijensia. Kwa ujumla, katika kipindi cha Septemba hadi Oktoba 2025 pekee, DCEA imekamata kilo 10,763.94 za dawa za kulevya, kilo 6,007 na lita 153 za kemikali bashirifu, huku watuhumiwa 89 wakikamatwa, na baadhi yao tayari wamefikishwa mahakamani.
Kamishna Lyimo alimalizia kwa kusema DCEA itaendelea na operesheni hizi bila kuchoka ili kuhakikisha Tanzania inabaki salama. "Tutaendelea kushirikiana na wananchi na wadau wote ili kuzuia vizazi vijavyo visiangamie kwa sumu ya dawa za kulevya," alisema.