Katika uamuzi muhimu wa kisheria, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imekubaliana na pingamizi lililowasilishwa na Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, dhidi ya ushahidi wa video katika kesi ya uhaini inayomkabili. Mahakama imebainisha kwamba shahidi wa tatu wa upande wa Jamhuri, ambaye ni mtaalamu wa picha, hana sifa za kisheria za kuwasilisha vielelezo vya video na kadi za kumbukumbu (memory card) mahakamani.
Uamuzi huo ulitolewa leo na Jopo la Majaji watatu lililoongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, akisaidiwa na Majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde, baada ya kupitia kwa kina hoja za pande zote mbili.
Tundu Lissu alipinga ushahidi wa Mkaguzi wa Polisi na Mtaalamu wa Uchunguzi wa Kielektroniki, Samwel Kaaya, akisisitiza kwamba shahidi huyo aliteuliwa kwa mujibu wa GN 745 ya Desemba 16, 2022, iliyotolewa chini ya Kifungu cha 216 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA). Kulingana na Lissu, uteuzi huo ulimruhusu Kaaya kushughulika na picha (photographs) pekee, na si picha za mjongeo (video) au masuala ya teknolojia ya kielektroniki (cyber).
Jaji Ndunguru alifafanua kwamba hoja kuu ilikuwa ni kama shahidi huyo anastahili kuwasilisha ushahidi huo kama mtaalamu au la. Hoja za utetezi wa Lissu zilionyesha kuwa video na picha za kawaida ni vitu viwili tofauti, na video zinahitaji utaalamu maalum wa kielektroniki unaokwenda mbali zaidi ya utaalamu wa picha zilizochapishwa.
Kwa upande wa Jamhuri, walijaribu kupinga pingamizi hilo, wakidai kuwa shahidi ana uwezo wa kitaalamu, alifanya uchunguzi, na kwamba video ni aina ya picha na tofauti si kubwa sana katika muktadha wa ushahidi wa kitaalamu.
Hata hivyo, baada ya uchambuzi wa kina, Mahakama ilikubaliana na hoja za Lissu. Jopo la Majaji lilibainisha kuwa Kifungu cha 216 cha CPA kinataja "picha" pekee na si "video". Mahakama ilieleza kuwa video zina mahitaji maalum ya kiteknolojia na zinachukuliwa kama ushahidi wa kielektroniki, ambao unahitaji mtaalamu mwenye utambuzi maalum katika fani hiyo, na sio tu mtaalamu wa picha.
"Shahidi ambaye ni mtaalamu wa picha hana uwezo wa kisheria kushughulikia video zinazohifadhiwa kwenye flash au memory card. Uteuzi wake haukumruhusu kuhusika na video, bali picha tu," alifafanua Jaji Ndunguru. Kutokana na uamuzi huo, Mahakama ilikubaliana na pingamizi hilo na kusisitiza kuwa flash disk na memory card zenye video za mjongeo havitakubaliwa kama ushahidi katika shauri hilo kupitia shahidi huyo. Hoja hiyo pekee ilitosha kutupilia mbali ombi la Jamhuri.