Kesi ya Uhaini: Lissu Aipa Jamhuri Pigo Nene, Ripoti ya Uchunguzi Yatupwa

economy | Thu Oct 23 2025


Kesi ya Uhaini: Lissu Aipa Jamhuri Pigo Nene, Ripoti ya Uchunguzi Yatupwa

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, amepata ushindi mwingine muhimu wa kisheria katika kesi ya uhaini inayomkabili, baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, kukubaliana na pingamizi la upande wake na kuukataa ushahidi muhimu uliowasilishwa na upande wa Jamhuri.


Uamuzi huo wa leo umetolewa na jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu, likiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, akisaidiana na Majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde. Jopo hilo limetupilia mbali ripoti ya uchunguzi iliyoandaliwa na Mkaguzi wa Polisi, Samwel Kaaya, ambayo upande wa mashtaka ulitaka kuitumia kama kielelezo dhidi ya Lissu.


Hoja kuu za ushindi wa Lissu zilijikita katika mambo mawili ya kisheria. Kwanza, upande wa utetezi ulifanikiwa kuishawishi Mahakama kwamba shahidi huyo wa Jamhuri (Kaaya) hakuwa na mamlaka ya kisheria ya kuandaa ripoti ya kitaalamu aliyoiwasilisha. Jaji Karayemaha, akisoma sehemu ya uamuzi huo, alifafanua kuwa ingawa Bw. Kaaya ana taaluma ya uchunguzi wa picha, hakuteuliwa mahakamani hapo kama mtaalamu wa masuala ya kihalifu ya kimtandao (cyber expert).


Mahakama ilieleza kuwa mamlaka ya kisheria ya shahidi huyo, kama yalivyofafanuliwa katika Tangazo la Serikali (GN) Na. 779, yalimpa jukumu la kuchunguza na kuhakiki picha mnato na kisha kuandaa "cheti cha uthibitisho" (certificate). Hata hivyo, badala ya cheti, shahidi huyo aliandaa "ripoti ya kitaalamu" (expert report), jambo ambalo Mahakama imesema halikuwa ndani ya uwezo wake kisheria kwa kesi hii.


Hoja ya pili iliyozima ushahidi huo ilihusu chanzo cha taarifa zenyewe. Mahakama ilikubaliana na hoja za Lissu kwamba vifaa vya kielektroniki, ikiwemo 'flash disk' na 'memory card', ambavyo vilidaiwa kuhifadhi picha zilizochunguzwa, vilishawahi kukataliwa hapo awali na Mahakama hiyo hiyo kutumika kama vielelezo halali.


Jaji Karayemaha alisisitiza kwamba kwa kuwa vifaa hivyo (chanzo cha ushahidi) havikuwa vimekubalika kisheria, hakuna msingi wowote wa kupokea taarifa yoyote (ripoti) inayotokana na vifaa hivyo. "Kwa kuwa vifaa hivyo havikukubalika kama vielelezo, hakuna sababu ya kupokea taarifa yoyote inayotokana navyo. Hivyo, kielelezo hiki hakiwezi kupokelewa," ilisema sehemu ya uamuzi.


Kutokana na uamuzi huo, Mahakama imeridhia pingamizi la Tundu Lissu na kuitupa ripoti hiyo, ikieleza wazi kuwa shahidi aliyeiandaa hakuwa na sifa za kisheria za kuitoa kama ushahidi wa kitaalamu mahakamani.


Bw. Lissu anakabiliwa na shtaka moja zito la uhaini, kinyume na kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu. Shitaka hili linahusiana na maneno anayodaiwa kuyatamka kuhusu kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika mwaka 2025.


Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, inadaiwa kuwa mnamo Aprili 3, 2025, akiwa jijini Dar es Salaam, Lissu alitoa kauli za uchochezi zilizolenga kushawishi umma kuzuia uchaguzi huo. Baadhi ya maneno anayodaiwa kuyatamka ni pamoja na: “Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli..., kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi... kwa hiyo tunaenda kukinukisha..., sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli...”


The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.