Kesi ya mashtaka ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, imechukua sura mpya, huku mivutano mikali ya kisheria ikitawala kuhusu upokeleaji wa vielelezo muhimu vya kielektroniki. Upande wa Jamhuri (Serikali) umesimama kidete mbele ya Mahakama, ukidai kuwa hoja na mapingamizi yanayowasilishwa na mshtakiwa ni mbinu za makusudi za kuchelewesha kesi na hazina msingi wowote wa kisheria.
Mvutano huo ulipamba moto jana mbele ya jopo la majaji watatu—Jaji Dustan Ndunguru akisaidiana na majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde—huku Wakili Mkuu wa Serikali, Nassoro Katuga, akiongoza shambulizi la hoja dhidi ya mapingamizi manne yaliyowasilishwa na Lissu. Kiini cha mzozo ni pingamizi la Lissu la kuzuia kupokewa kwa 'flash diski' na 'memory cards' ambazo zina video zinazodaiwa kumuonesha akitoa maneno ya uhaini.
Wakili Katuga alieleza kushangazwa kwake na msimamo wa Lissu. Alidai kuwa mshtakiwa huyo anajipinga, kwani awali alikuwa akitamka hadharani kuwa vielelezo hivyo viletwe mahakamani na kwamba hana shida navyo wala hatavipnga. Sasa, anapinga vikali visipokewe.
Katika kujibu hoja ya Lissu kwamba shahidi wa upande wa mashtaka, Mkaguzi wa Polisi na Mtaalamu wa Uchunguzi wa Kielektroniki, Samwel Kaaya, hana sifa za kitaalamu za kuwasilisha picha (video), Wakili Katuga alipuuzilia mbali hoja hiyo. Alisema Pw3 (Kaaya) alijipambanua kitaaluma, alieleza elimu na uzoefu wake, na alieleza jinsi alivyofanyia kazi vielelezo hivyo na kutoa maoni yake ya kitaalamu kuwa video aliyoikagua ni halisi na haijahaririwa.
Hoja nyingine nzito ilikuwa madai ya Lissu kwamba vielelezo hivyo vilikiuka Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA) kwa kutokusomwa au kuoneshwa wakati wa hatua ya awali ya kesi (Committal proceedings) katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Hapa, Wakili Katuga alimshutumu Lissu kwa kile alichokiita "kusema uongo" mbele ya mahakama. Katuga aliwaalika majaji kuzama kwenye kumbukumbu za mwenendo wa kesi kutoka Mahakama ya Kisutu, akitaja ukurasa wa 92 na 93, ambao alidai unaonesha wazi kuwa vielelezo hivyo vilitajwa na kusomwa.
"Alitushtusha," alisema Wakili Katuga, "Tuwe 'noted' kwamba wakati mtu anajitetea anaweza kwenda mbali sana kwa kusema uongo, sisemi haya kwa kujifurahisha. Ninawaalika kwenye Committal proceedings ukurasa wa 92... hakuwaalika kwa kuangalia uongo wake." Aliongeza kuwa katika ukurasa wa 97, Lissu mwenyewe alinukuliwa akikiri kusema maneno hayo kwenye mkutano wa wazi.
Kuhusu hoja kwamba ripoti ya mtaalamu (Kaaya) ilitakiwa kutangulia kabla ya vielelezo vyenyewe (flashi), Wakili Katuga alitumia msemo wa Lissu mwenyewe kumjibu. Alisema hoja hiyo ni sawa na "kutanguliza mkokoteni mbele halafu wanataka punda asukume mkokoteni huo," akimaanisha ni hoja isiyo na mantiki.
Vilevile, pingamizi la nne la Lissu kuhusu kuvunjika kwa mnyororo wa utunzaji wa vielelezo (chain of custody), Wakili Katuga aliliona kama hoja "hafifu" ya kisheria. Alisema, akirejea maamuzi ya Mahakama ya Rufani, kwamba hata kama mnyororo huo ukikatika, si sababu ya kuzuia kielelezo kupokewa, bali ni jukumu la mahakama baadaye kuamua uzito wa kielelezo hicho.
"Hii ni hoja hafifu ya kisheria... Imeletwa kwa kubahatisha na kupoteza muda wa mahakama. Tunaomba mlitupilie mbali mapingamizi yote manne," alihitimisha Katuga.
Hata hivyo, Lissu aliposimama kwa majibu ya mwisho (rejoinder), aliendelea kusisitiza kuwa video hizo hazikuoneshwa Kisutu na kuomba mahakama izitupilie mbali. Baada ya kusikiliza vuta ni kuvute hiyo ya kisheria, Mahakama iliahirisha kesi hiyo hadi kesho, Oktoba 22, 2025, ili kufanya utafiti wa kina juu ya hoja zilizowasilishwa kabla ya kutoa uamuzi wake.