Mvutano Mkali Kesi ya Lissu: Serikali Yakana Ushahidi wa Shahidi Wake, Lissu Acharuka

politics | Fri Oct 10 2025


Mvutano Mkali Kesi ya Lissu: Serikali Yakana Ushahidi wa Shahidi Wake, Lissu Acharuka

Mabishano makali ya kisheria yameibuka katika Mahakama Kuu kwenye kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, baada ya upande wa Jamhuri kuweka pingamizi zito dhidi ya ombi la mshtakiwa kutumia maelezo ya shahidi wa mashtaka kama kielelezo cha utetezi. Hali hiyo ilimlazimu Lissu kutoa kauli kali, akidai kuwa mawakili wa Serikali wanataka "kula keki yao na wakati huo huo waibakize," akimaanisha wanampa utaratibu wa kufuata kisha wanamgeuka.


Mzozo huo ulianza pale Lissu alipoliomba jopo la majaji watatu, linaloongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, kumwamuru shahidi wa upande wa mashtaka, Mkaguzi wa Polisi John Kaaya, awasilishe mahakamani maelezo yake aliyoyatoa awali. Lengo la Lissu lilikuwa ni kutumia maelezo hayo kuonyesha mkinzano na ushahidi anaoutoa shahidi huyo mahakamani, na hivyo kuhoji kuaminika kwake.


Hata hivyo, Wakili wa Serikali Mkuu, Ajuaye Zegeli, alisimama kidete kupinga ombi hilo, akidai kuwa Lissu hakufuata utaratibu sahihi wa kisheria. Zegeli alisisitiza kuwa, kwa mujibu wa sheria, mshtakiwa alipaswa kwanza kumdondosa shahidi kwa kumuuliza maswali kuhusu maeneo mahususi yenye utata na mkinzano katika maelezo yake, na ndipo aombe sehemu hizo tu zipokelewe kama kielelezo, na si maelezo yote. "Kwa mtazamo wetu, ameshindwa kuielekeza Mahakama ipasavyo na hajamuhoji shahidi kwenye maeneo yenye mkinzano kama taratibu zinavyotaka," alisisitiza Zegeli.


Hoja hiyo iliungwa mkono na Wakili wa Serikali Mkuu, Ignas Mwinuka, aliyedai kuwa ni shahidi mwenyewe ndiye anayepaswa kuomba kutoa maelezo yake kama kielelezo, na si mshtakiwa.


Akijibu mapigo, Lissu alieleza kuwa alifuata maelekezo aliyopewa na upande wa Jamhuri hapo awali kuhusu utaratibu huo. Alirejea maamuzi ya Mahakama ya Rufani katika kesi za Lilian Jesus Fotes na Shadrack Sospiter, akisema msimamo wa kisheria unaotambulika ni kwamba, maelezo ya shahidi husomwa kwanza, kisha yanapokelewa kama kielelezo, na baada ya hapo ndipo shahidi anaweza kuhojiwa kwa kina kuhusu mkinzano uliopo. "Huwezi kumdodosa shahidi kabla maelezo hayajapokelewa. Waheshimiwa majaji, sheria ziko wazi hapa nchini, msikubali kupelekwa India," Lissu alisisitiza, akiiomba mahakama kutupilia mbali pingamizi hilo.


Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, jopo la majaji limeahirisha kesi hiyo hadi Jumatatu asubuhi, ambapo litatoa uamuzi kuhusu pingamizi hilo kabla ya kuendelea na usikilizwaji.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.