Ulaya Yasalimu Amri kwa Vigogo wa Marekani: Yalegeza Sheria za AI na Data ili 'Kushindana'

it | Fri Nov 21 2025


Ulaya Yasalimu Amri kwa Vigogo wa Marekani: Yalegeza Sheria za AI na Data ili 'Kushindana'

Umoja wa Ulaya (EU), ambao kwa miaka mingi umesimama kama "Polisi wa Dunia" linapokuja suala la kulinda data za watumiaji wa mtandao na kudhibiti makampuni ya teknolojia, umeonekana kulegeza kamba kwa ghafla. Katika hatua iliyowashangaza wengi na kuwakasirisha wanaharakati wa haki za binadamu, EU imetangaza kifurushi kipya cha sheria kinachoitwa 'Digital Omnibus' ambacho kimsingi kinarahisisha mambo kwa makampuni makubwa ya teknolojia (Big Tech) kama Google na Meta.


Uamuzi huu unatafsiriwa na wachambuzi wa mambo kama "usaliti" au "kusalimu amri" mbele ya shinikizo kali kutoka kwa Marekani, utawala wa Rais Donald Trump, na hofu ya Ulaya kuachwa nyuma kiuchumi katika mapinduzi ya Akili Mnemba (AI).


'Likizo' ya Miezi 16 kwa AI


Mabadiliko makubwa zaidi ni kuahirishwa kwa utekelezaji wa sheria kali za kudhibiti mifumo hatarishi ya AI (High-risk AI regulation). Awali, sheria hizi zilipangwa kuanza kung'ata mwezi Agosti 2026. Lakini sasa, Tume ya Ulaya imesogeza tarehe hiyo mbele kwa miezi 16, hadi Desemba 2027. Hii inawapa watengenezaji wa AI "muda wa kupumua" wa kuendelea na shughuli zao bila kubanwa mbavu na serikali.


Pia, wamepunguza urasimu kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati kwa kupunguza mzigo wa kuandaa nyaraka na kurahisisha njia za kuomba idhini ya 'cookies' mtandaoni—kile kidude kinachokera unapoingia kwenye tovuti na kukulazimisha ukubali masharti.


Data Zenu Sasa ni 'Mali ya Umma'?


Eneo lililozua gumzo zaidi ni kulegezwa kwa sheria maarufu ya GDPR (General Data Protection Regulation). Hii ndiyo sheria iliyokuwa ikiiogofya dunia na hata kutumiwa kama kielelezo na nchi nyingi, ikiwemo Tanzania wakati wa kutunga Sheria yetu ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.


Katika mpango huu mpya, EU imependekeza kuwa data ambazo "zimefichwa utambulisho" (anonymized data) hazitahesabiwa tena kama taarifa binafsi. Hii ni 'keki' kwa makampuni ya AI, kwani inawapa uhalali wa kuchota data za raia wa Ulaya na kuzitumia kufundisha mifumo yao ya AI bila hofu ya kupigwa faini kubwa, mradi tu majina ya watu yameondolewa.


Sababu ya Kubadili Gia Angani


Kwanini Ulaya imebadilika ghafla? Kamishna wa Uchumi wa EU, Valdis Dombrovskis, alijibu swali hili kwa uwazi: "Ulaya haijafaidika vya kutosha na mapinduzi ya kidijitali... hatuwezi kushindwa kwenda na wakati."


Ukweli mchungu ni kwamba Ulaya inahisi inapitwa na Marekani na China. Wamegundua kuwa sheria zao kali zinakimbiza wawekezaji na kuua ubunifu. Shinikizo kutoka kwa makampuni ya teknolojia na utawala wa Marekani limekuwa likisema wazi: "Sheria zenu zinaua biashara." Inaonekana Ulaya wameamua kuwa ni bora kuwa na teknolojia kuliko kuwa na sheria kali zinazowaacha nyuma kimaendeleo.


Wanaharakati Wakaa Mguu Pande


Hata hivyo, hatua hii haijapokelewa vyema na watetezi wa haki za faragha. Muungano wa mashirika 127 ya kiraia umetoa barua kali ya wazi, ukiita hatua hii kuwa ni "kurudi nyuma kukubwa zaidi kwa haki za kidijitali katika historia ya EU."


Maandamano yamezuka katika mitaa ya Brussels, makao makuu ya EU, huku waandamanaji wakidai kuwa viongozi wao wamekubali "kugoti" mbele ya matakwa ya makampuni ya Marekani kwa gharama ya faragha ya raia wao. Wanahofia kuwa uhuru wa kutumia data kiholela utawapa nguvu kubwa makampuni kama Meta na Google kuwapeleleza watu na kutengeneza faida bila kutoa ulinzi wa kutosha.


Kwa Tanzania na nchi nyingine zinazoendelea, hii ni funzo muhimu. Wakati tunajifunza kutoka kwa sheria za Ulaya, tunaona jinsi ambavyo hata wao wanalazimika kurekebisha msimamo ili wasiachwe nyuma kiuchumi na teknolojia mpya za AI.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.