Fagio la Chuma Ulaya: Watoto Chini ya Miaka 13 Marufuku Mitandaoni na AI, Wazazi Wapewa Nguvu Mpya

it | Fri Nov 28 2025


Fagio la Chuma Ulaya: Watoto Chini ya Miaka 13 Marufuku Mitandaoni na AI, Wazazi Wapewa Nguvu Mpya

Dunia imeanza kuamka kutoka usingizini na kutambua kuwa simu janja na mitandao ya kijamii si "malaika" kwa watoto wetu. Katika hatua ya kihistoria inayolenga kulinda kizazi kijacho dhidi ya "sumu" ya kidijitali, Bunge la Umoja wa Ulaya (EU) limepitisha azimio zito linalopiga marufuku watoto wenye umri chini ya miaka 13 kutumia mitandao ya kijamii na roboti za Akili Mnemba (AI Chatbots).


Azimio hili, ambalo limeungwa mkono kwa kishindo na wabunge 483 dhidi ya 92 waliopinga, linatoa ujumbe mzito kwa makampuni makubwa ya teknolojia kama Meta (Facebook/Instagram), TikTok, na OpenAI: "Watoto wetu si bidhaa ya biashara yenu."


Sheria Mpya: Miaka 13 Ndio Mwisho wa Mchezo


Kwa mujibu wa wabunge hao walioketi Strasbourg, Ufaransa, mpango huo unataka kuweka 'Red Line' (Mstari Mwekundu) wa umri wa miaka 16 kama kiwango cha chini cha matumizi huru ya mitandao.


Mchanganuo uko hivi:

  1. Chini ya Miaka 13: Ni marufuku kabisa (Total Ban). Mtoto haruhusiwi kuwa na akaunti ya TikTok, Instagram, wala kucheza na AI Chatbots. Hii ni sawa na jinsi mtoto haruhusiwi kuingia baa.
  2. Kati ya Miaka 13 na 16: Mtoto ataruhusiwa kutumia mitandao hii TU kama atakuwa na idhini maalum kutoka kwa wazazi au walezi (Parental Consent).


Lengo la azimio hili ni kuondoa mkanganyiko wa sheria tofauti tofauti ndani ya nchi wanachama wa EU na kuwa na sheria moja ngumu itakayolinda watoto wote barani humo.


Vita Dhidi ya Uraibu na Matangazo ya Ulaghai


Hoja kuu iliyoendesha maamuzi haya ni afya ya akili ya watoto. Wabunge wamekerwa na mitandao inayotumia mbinu za kisaikolojia (addictive design) kuwafanya watoto wagande kwenye vioo vya simu kwa masaa mengi, kama vile wanavyofanya waraibu wa dawa za kulevya au kamari.


Azimio hilo linataka kupiga marufuku matangazo yanayolenga kuwahadaa watoto (manipulative ads) na vipengele vinavyochezea akili zao ili wasitoke mtandaoni. Aidha, tovuti zote zitakazokaidi sheria hizi mpya zinakabiliwa na tishio la kufungiwa kabisa (blocked) barani Ulaya. Pia, kuna msisitizo mkubwa wa kudhibiti taarifa za uongo (fake news) zinazozalishwa na AI ambazo zinaweza kupotosha akili changa.


Safari Bado ni Ndefu


Hata hivyo, ni muhimu kufahamu kuwa hili bado ni azimio la Bunge (Resolution) na si sheria kamili yenye nguvu ya kisheria papo hapo. Ili iwe sheria inayong'ata, Tume ya Ulaya (European Commission) inatakiwa kuandaa muswada rasmi, na kisha nchi wanachama zikubaliane. Mchakato huu unaweza kuchukua miaka kadhaa, lakini "fimbo imeshaonekana."


Dunia Yote Imeungana: Australia na Marekani Pia


Umoja wa Ulaya hauko peke yake katika vita hii. Hivi karibuni, Serikali ya Australia ilitangaza mpango wa kupiga marufuku mitandao ya kijamii kwa watoto chini ya miaka 16 kuanzia mwezi ujao. Nchi ya Malaysia nayo imetangaza kufuata nyayo hizo kuanzia mwaka 2026.


Hata huko Marekani, mambo yameanza kubadilika. Kampuni maarufu ya Character.AI, ambayo inatengeneza roboti za kuongea na watu, imeamua yenyewe (self-regulation) kuzuia watoto chini ya miaka 18 kutumia huduma zao kuanzia tarehe 26 mwezi huu. Hii ni mara ya kwanza kwa kampuni kubwa ya AI kuchukua hatua ya kujidhibiti namna hii.


Kwa wazazi wa Kitanzania, huu ni mjadala tunaopaswa kuufuatilia kwa karibu. Wakati mataifa yaliyoendelea yakichukua hatua kali kudhibiti watoto wao mitandaoni, sisi bado tunawaachia simu kama "yaya" wa kuwanyamazisha wanapolia? Kama wahenga wasemavyo, "Samaki mkunje angali mbichi," na inaonekana dunia imeamua kumkunja samaki huyu wa kidijitali kabla hajateketeza kizazi kizima.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.