Umoja wa Ulaya (EU) kwa miaka mingi umekuwa maarufu na kutambulika duniani kote kwa sheria yake kali zaidi ya kulinda data na faragha ya watu mtandaoni, inayojulikana kwa kifupi cha 'GDPR' (General Data Protection Regulation). Hii ndiyo sheria iliyoyatikisa makampuni makubwa kama Google na Meta (Facebook) na kuwalazimisha kukuomba "ukubali 'cookies'" kila unapotembelea tovuti.
Lakini sasa, inaonekana ngome hiyo imara ya ulinzi iko mbioni kubomolewa, na chanzo ni presha kubwa kutoka kwa 'mungu mpya' wa teknolojia: Akili Mnemba (Artificial Intelligence - AI).
Taarifa zilizovuja kutoka Brussels, makao makuu ya EU, zinaonyesha kuwa Tume ya Ulaya inapanga kufanya mabadiliko makubwa na ya kushangaza kwenye sheria hiyo ili kurahisisha maisha kwa watengenezaji wa programu za AI. Hii inafuatia habari za awali kwamba EU pia inalegeza msimamo wake kwenye 'Sheria ya AI' (AI Act) baada ya shinikizo kali kutoka kwa utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani na makampuni makubwa ya teknolojia (Big Tech).
Mabadiliko yaliyopendekezwa kwenye GDPR yanatisha. Mpango huo unalenga kuunda "msamaha maalum" kwa kampuni za AI. Msamaha huu utawapa uhalali wa kisheria wa kutumia 'data nyeti'—kama vile maoni yako ya kisiasa, imani yako ya kidini, na hata taarifa zako za kiafya—kwa ajili ya kufundisha na kuboresha mifumo yao ya AI. Zaidi ya hayo, wanapanga kubadilisha maana ya 'data binafsi' ni nini na kupunguza ulinzi kwa data ambazo tayari "zimefichwa utambulisho" (anonymized data).
Sababu kuu ya mabadiliko haya ya ghafla ni hofu ya kiuchumi. Wakati Marekani na China zikikimbia kwa kasi kwenye mbio za AI, Ulaya inajiona imeachwa nyuma. Ripoti ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Italia, Mario Draghi, ilionya waziwazi kwamba sheria kali za GDPR, ingawa zilikuwa na nia njema, sasa zinaua uvumbuzi na kudhoofisha ushindani wa Ulaya katika sekta ya AI.
GDPR haikuwa sheria ya mchezo. Tangu ilipoanza kutumika mwaka 2018, imekuwa mwiba mkali kwa makampuni ya teknolojia. Sheria hiyo inatoza faini ya hadi Euro milioni 20 (kama Shilingi bilioni 56 za Kitanzania) au 4% ya mapato yote ya kampuni duniani—chochote kilicho kikubwa zaidi. Hii ndiyo sababu Google na Meta zimepigwa faini za mabilioni na ndiyo sababu kampuni kama Meta na 'X' (zamani Twitter) zilichelewa kuzindua huduma zao za AI barani Ulaya, zikihofia adhabu hizo kali.
Kama ilivyotarajiwa, mpango huu mpya umezua tufani la kisiasa. Watu walioitunga sheria hiyo wamekasirika. Jan Philipp Albrecht, mwanasiasa wa Ujerumani na mmoja wa "wabunifu" wakuu wa GDPR, amehoji kwa hasira: "Huu ndio mwisho wa ulinzi wa data na faragha barani Ulaya?"
Mwanaharakati mwingine maarufu wa faragha, Max Schrems wa kikundi cha Noyb, ameitaja mipango hii kuwa "ya kutisha na iliyopikwa hovyo," akionya kuwa italeta madhara makubwa kwa raia.
Rasimu hii inatarajiwa kuwekwa hadharani rasmi tarehe 19 Novemba. Baada ya hapo, italazimika kupitishwa na nchi zote wanachama wa EU na Bunge la Ulaya, ambapo tayari kuna mgawanyiko mkubwa wa maoni. Vita kati ya hitaji la kulinda siri za raia na tamaa ya kutawala mapinduzi ya AI ndiyo kwanza imeanza.