Makampuni makubwa zaidi ya teknolojia duniani, yakiwemo Meta (wamiliki wa Instagram), TikTok, na Google, yameanza kutekeleza sera na vipengele vipya vikali vinavyolenga kuongeza usalama na ulinzi kwa watumiaji vijana (matineja) katika majukwaa yao. Hatua hizi zinakuja kufuatia shinikizo kubwa kutoka kwa jamii na serikali duniani kote, zinazoyataka makampuni haya kuwajibika zaidi kwa usalama wa watumiaji wao walio katika umri mdogo.
Meta Yaongeza Ulinzi Kwenye 'DM' za Instagram
Kampuni ya Meta imetangaza vipengele vipya vya usalama katika sehemu ya kutuma ujumbe wa faragha (Direct Message - DM) kwa akaunti za vijana (wenye umri wa miaka 13-17). Sasa, kijana anapopiga soga na mtu kwenye DM, ataweza kuona maelezo muhimu kuhusu akaunti ya mtu huyo, ikiwemo ni lini akaunti hiyo ilifunguliwa (mwaka na mwezi). Lengo ni kumpa kijana taarifa zaidi zitakazomsaidia kutambua akaunti mpya au za kutiliwa shaka. Zaidi ya hayo, Instagram imerahisisha mchakato wa kumzuia (block) na kuripoti mtu kwa kuweka vitufe hivyo pamoja sehemu moja.
TikTok Yaimarisha Udhibiti wa Wazazi
Jukwaa la video fupi la TikTok nalo limeongeza nguvu kwa wazazi katika kulinda watoto wao. Sasa, wazazi wanaweza kupokea taarifa papo kwa papo kwenye simu zao kila wakati mtoto wao anapopakia picha au video. Vilevile, wazazi wamepewa uwezo wa kudhibiti mambo mbalimbali kama vile mipangilio ya faragha ya mtoto, aina ya mada anazopenda kuangalia, ruhusa ya kupakua maudhui, na hata orodha ya watu anaowafuata (following). Hii ni pamoja na sera ya TikTok iliyopo ya kuweka kikomo cha saa moja (dakika 60) cha matumizi kwa siku kwa vijana walio chini ya miaka 18.
Google Yaweka Ulinzi wa Kiotomatiki
Google imetangaza kuwa itaanza kutumia teknolojia yake kutambua watumiaji walio chini ya umri wa miaka 18 na kuwasha kiotomatiki mipangilio ya ulinzi katika huduma zake zote. Hii ina maana kuwa kijana anapotumia huduma za Google, atalindwa kiotomatiki na mipangilio ya usalama, na wazazi wao watapata fursa ya usimamizi na udhibiti. Sera hii itaanza kwa watumiaji wachache nchini Marekani na kisha kusambazwa taratibu duniani kote.
Shinikizo la Kimataifa
Hatua hizi za makampuni ya teknolojia zinachochewa na wimbi la sheria na kanuni zinazopitishwa na serikali mbalimbali. Kwa mfano, nchini Australia, sheria mpya ilipitishwa mwaka jana inayopiga marufuku matumizi ya mitandao ya kijamii kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 16, na inatarajiwa kuanza kutumika Desemba mwaka huu.
Afisa mmoja kutoka sekta ya teknolojia alieleza, "Aina za uhalifu na maudhui hatari mtandaoni zinabadilika na kuongezeka kwa kasi. Makampuni yanajitahidi kwenda sambamba na mabadiliko haya na kutimiza matarajio ya jamii katika kulinda watumiaji."