Hatimaye lile wingu jeusi lililokuwa likitanda nchini Australia kuhusu matumizi ya mitandao ya kijamii kwa watoto limeanza kunyesha leo. Katika hatua ambayo inaweza kutajwa kama mapinduzi ya kwanza ya aina yake duniani, Serikali ya Australia imeamua "kufunga vioo" rasmi kuanzia leo tarehe 10, kwa kupiga marufuku matumizi ya mitandao ya kijamii kwa vijana wote wenye umri chini ya miaka 16.
Sheria hii mpya na kali, ambayo imezua mjadala mzito duniani kote, inalenga mitandao kumi mikubwa inayoongoza kwa kuvuta hisia za 'Kizazi cha Dotcom'. Orodha hiyo inajumuisha vigogo kama Facebook, Instagram, Threads, YouTube, TikTok, X (zamani Twitter), Snapchat, Reddit, Twitch, na Kick. Hii ina maana kuwa kuanzia sasa, Australia imekuwa nchi ya kwanza duniani kuchukua hatua ya kisheria 'kuwapokonya simu' watoto kidijitali ili kulinda afya zao za akili.
'Kisu Kikali' kwa Kampuni za Mitandao
Kulingana na sheria hiyo mpya, jukumu la kusafisha akaunti za watoto halipo kwa wazazi pekee, bali 'mzigo' huo umetwishwa mabegani mwa wamiliki wa mitandao hiyo. Kampuni hizo zimeamriwa kufuta au kuzima (deactivate) akaunti zote za watoto waliopo chini ya miaka 16 na kuhakikisha hakuna akaunti mpya zinazofunguliwa na kundi hilo.
Serikali ya Australia haitanii katika hili. Imeelezwa kuwa kampuni yoyote itakayoshindwa kuweka mifumo madhubuti ya kuwadhibiti watoto hao itakumbana na 'mkono mrefu wa sheria' kwa kutozwa faini ya kufuru ya Dola za Australia milioni 49.5, ambayo ni sawa na takriban Shilingi za Kitanzania Bilioni 91.5. Hiki ni kiasi ambacho kinaweza kutetemesha hata kampuni kubwa za teknolojia.
Vita Dhidi ya 'Uteja' wa Algorithm
Hata hivyo, serikali imeweka wazi kuwa lengo si kuwanyima watoto haki ya kupata taarifa, bali kuwakinga na madhara ya 'algorithms' zinazojenga uraibu. Kwa mantiki hiyo, mtoto chini ya miaka 16 bado ataweza kuingia YouTube na kutazama video, lakini hataruhusiwa kuwa na akaunti (Log in).
Hii inamaanisha hawatapata zile 'notification' zinazowafanya washinde kwenye simu, hawatatoa 'likes', wala kuingia kwenye mitego ya algorithm inayowasoma tabia zao na kuwaletea maudhui yanayoweza kuharibu kisaikolojia. Taasisi ya Kusimamia Usalama Mtandaoni ya Australia (eSafety) imebainisha kuwa hali ilikuwa mbaya, kwani asilimia 96 ya vijana chini ya miaka 16 nchini humo (takriban watoto Milioni 1) wanamiliki akaunti za mitandao ya kijamii, jambo lililokuwa likihatarisha makuzi yao.
Mtihani wa Vitambulisho: Nani Mkubwa, Nani Mdogo?
Licha ya nia njema hiyo, utekelezaji wa sheria hii unakabiliwa na changamoto inayofanana na 'kudaka maji kwa kiganja'. Tofauti na Tanzania ambapo tuna vitambulisho vya NIDA au Korea yenye mfumo wa namba za utambulisho, Australia haina mfumo wa vitambulisho vya taifa kwa kila mwananchi. Hii inazua swali gumu: Mitandao itajuaje huyu ana miaka 15 na yule ana 17?
Mbinu mbalimbali zinapendekezwa, ikiwemo kutumia pasipoti, leseni za udereva, au hata teknolojia ya kisasa ya Akili Mnemba (AI) inayotambua umri kwa kuscan sura. Hata hivyo, wadau wa haki za faragha wameonya juu ya usalama wa taarifa hizo. Serikali imekiri kuwa kunaweza kuwa na makosa ya kiufundi mwanzoni na imeagiza majukwaa hayo kurekebisha changamoto hizo pindi zinapojitokeza ili kutokuingilia uhuru wa watu wazima.
Dunia Inatazama
Australia haiko peke yake katika vita hii ya kimaadili. Bunge la Umoja wa Ulaya (EU) hivi karibuni lilipitisha azimio la kutaka watoto chini ya miaka 16 wapate ridhaa ya wazazi kabla ya kutumia mitandao. Nchi nyingine kama New Zealand, Malaysia, na Singapore nazo zipo mbioni kutunga sheria kama hizi. Je, wimbi hili la ulinzi wa watoto litafika Afrika Mashariki hivi karibuni? Muda utatuambia.