Wimbi la mabadiliko makubwa linakumba wafanyakazi katika makampuni makubwa ya teknolojia duniani. Kampuni ya Meta, ambayo inamiliki mitandao ya Facebook, Instagram, na WhatsApp, imetangaza rasmi kuwa inabadilisha vigezo vyake vya kupima utendaji kazi wa wafanyakazi, na sasa matumizi ya Akili Mnemba (AI) yatakuwa ni sehemu muhimu ya tathmini hiyo.
Katika barua pepe iliyotumwa kwa wafanyakazi wote Novemba 13, Mkuu wa Rasilimali Watu wa Meta, Janelle Gale, aliweka wazi kuwa kuanzia mwaka 2026, "mchango unaotokana na matumizi ya AI" utakuwa ni moja ya "matarajio ya msingi" katika tathmini ya kila mfanyakazi. Hii ina maana kwamba mfanyakazi ambaye hataweza kuonyesha jinsi alivyotumia AI kuboresha kazi yake atakuwa katika hatari ya kupata alama za chini kwenye tathmini yake ya kila mwaka.
Adhabu na Zawadi Zaanza Mwaka Huu (2025)
Ingawa sheria hiyo itaanza rasmi mwaka 2026, Meta imeanza kuitekeleza kwa njia isiyo ya moja kwa moja kuanzia sasa. Katika tathmini za utendaji kazi za mwaka huu wa 2025, ingawa hakuna adhabu rasmi kwa kutotumia AI, wafanyakazi wote wametakiwa kujumuisha kwenye ripoti zao za kujitathmini (self-evaluation) jinsi walivyotumia zana za AI (kama msaidizi wao wa ndani 'Metamate' au 'Gemini' ya Google) kuboresha utendaji wao.
Muhimu zaidi, Janelle Gale alisisitiza kwamba kwa mwaka huu wa 2025, wale wafanyakazi watakaoonyesha "ufanisi wa kipekee" katika kutumia AI kuongeza tija kazini watapata zawadi maalum na bonasi. Hii ni ishara tosha kwamba ingawa hakuna adhabu rasmi bado, mbio za nani ni bora katika kutumia AI zimeanza rasmi ndani ya Meta.
Hali Ikoje kwa Makampuni Mengine?
Meta haiko peke yake katika hili. Huu ni mwelekeo unaoshika kasi kote Silicon Valley:
- Microsoft: Tangu mwezi Juni, kampuni hii ilishaanza kuwasisitizia wafanyakazi wake kutumia zana za AI, ikisema wazi kwamba "kutumia AI si jambo la hiari tena." Baadhi ya idara tayari zinapanga kuingiza kipengele hiki kwenye tathmini rasmi za utendaji.
- Google: Mkurugenzi Mtendaji, Sundar Pichai, alitoa ujumbe kama huo mwezi Julai, akisema ili kampuni iweze kuongoza mapinduzi ya AI, ni lazima wafanyakazi wake wawe mstari wa mbele kuitumia.
Wakati Wengine Wakipima, Wengine Wanafukuza
Wakati Meta na Google zikionekana kutoa motisha na kuweka vigezo vya upimaji, makampuni mengine yamechukua hatua kali zaidi: kufukuza wale wasioendana na kasi.
- Accenture: Kampuni hii kubwa ya ushauri wa kibiashara iliweka mambo wazi kabisa. Mkurugenzi wao Mkuu, Julie Sweet, aliwaambia wawekezaji kwamba ingawa wamefunza wafanyakazi wao 779,000 mbinu za AI, "kwa wafanyakazi ambao mafunzo hayo si jambo la kweli kwao (yaani hawawezi kujifunza), watafutwa kazi."
- Amazon: Mwezi uliopita, kampuni hii ilitangaza kupunguza wafanyakazi 14,000 kutokana na ujio wa AI. Mkurugenzi Mkuu, Andy Jassy, alisisitiza kuwa "AI itapunguza baadhi ya kazi zinazofanywa na binadamu leo," na kwamba kampuni lazima iongeze kasi ya kufanya kazi zake kiotomatiki.
Ujumbe kutoka kwa makampuni haya makubwa uko wazi: zama za kufanya kazi bila kutumia AI zinakaribia mwisho. Ujuzi wa kutumia zana hizi sasa unageuka kutoka kuwa faida ya ziada na kuwa hitaji la lazima ili kuweza kubaki na ajira.