Hali ya hewa imezidi kuchafuka katika medani za kidiplomasia na kiuchumi barani Ulaya. Katika kile kinachoonekana kama "kutiana vidole machoni," Serikali ya Urusi imetoa onyo zito na la "kufa mtu" kwa Umoja wa Ulaya (EU), ikisema kuwa jaribio lolote la kutumia mali zake zilizozuiwa (frozen assets) kuisaidia Ukraine litatafsiriwa kama wizi wa mchana kweupe na litaleta maafa makubwa kwenye mfumo wa fedha duniani.
Mzozo huu mpya umepamba moto baada ya Umoja wa Ulaya kutangaza mpango kabambe wa kutaka kuzitumia mali za Urusi zilizoshikiliwa barani humo ili kuikopesha au kuipa Ukraine msaada wa fedha kiasi cha Euro bilioni 90 (Takriban Shilingi za Kitanzania Trilioni 270). Fedha hizi zinakusudiwa kuisaidia Ukraine ambayo imeyumba kiuchumi kutokana na vita vinavyoendelea kwa zaidi ya miaka miwili sasa.
Akiwasha moto huo wa maneno, Balozi wa Urusi nchini Ujerumani, Sergey Nechayev, amesema wazi kuwa kitendo hicho ni "uhuni wa kisheria." Katika mahojiano yake na shirika la habari la AFP, Balozi huyo alisisitiza kuwa kutumia mali za taifa lingine bila ridhaa ni wizi, na EU inapaswa kujiandaa kwa "mvua ya mashtaka" isiyo na kikomo endapo watathubutu kufanya hivyo.
"Huku ni kujichimbia kaburi wenyewe. EU itapoteza heshima yake yote ya kibiashara (business reputation). Wawekezaji wataogopa kuweka pesa Ulaya wakijua zinaweza kuporwa muda wowote. Hii itakuwa ni vurugu tupu kwenye mfumo wa fedha wa kimataifa," alionya Nechayev huku akisisitiza kuwa Ujerumani na Ubelgiji zinajua fika hatari hiyo.
Kiini cha mzozo huu kipo nchini Ubelgiji. Sehemu kubwa ya mali za Urusi zilizozuiwa ziko chini ya taasisi ya *Euroclear* yenye makao yake makuu Brussels. Serikali ya Ubelgiji, ikijua kuwa "ngoma nzito haibebwi kwa, haraka," imekuwa ikisita kuruhusu mali hizo kuguswa. Wabelgiji wanahofia kuwa wakiruhusu uporaji huo, watajitwika mzigo wa kesi za kisheria kwa miongo ijayo na wanaweza kukabiliwa na kisasi kikali kutoka kwa Urusi.
Hata hivyo, vigogo wa EU hawataki kusikia la mkuu wala la mdogo. Kansela wa Ujerumani, Friedrich Merz, alilazimika kutua Brussels usiku wa manane kufanya kikao kizito na Waziri Mkuu wa Ubelgiji, Bart De Wever. Lengo lilikuwa ni kumshawishi Mbelgiji huyo "alegeze kamba" kabla ya mkutano mkuu wa viongozi wa EU unaotarajiwa kufanyika tarehe 18 na 19 mwezi huu.
Licha ya mazungumzo hayo kutajwa kuwa "ya kujenga," taarifa za ndani zinaeleza kuwa Ubelgiji bado ina kigugumizi. Wana hofu kuwa Urusi haitakaa kimya. Imebainika kuwa endapo EU itatumia mabavu kuchukua fedha hizo, Urusi inapanga kufungua mashtaka kupitia Mahakama za Hong Kong. Kwa kuwa Hong Kong ipo chini ya ushawishi wa China (ambayo ni rafiki wa Urusi), kuna uwezekano mkubwa EU ikapigwa faini kubwa au mali zake zilizoko Asia zikakamatwa kufidia hasara hiyo.
Balozi Nechayev hakusita pia kutoa dhihaka kwa EU, akisema kuwa hatua hii ya kutaka kuiba mali za Urusi ni ishara tosha kuwa Ulaya imefilisika na haina tena uwezo wa kuisaidia Ukraine kwa pesa zake yenyewe. "Wameishiwa pumzi, sasa wanataka kutumia mali zetu kufadhili vita dhidi yetu, jambo ambalo halikubaliki hata kidogo," alimailizia.
Vita hii ya kiuchumi inaweka rehani uaminifu wa mabenki na taasisi za fedha za Magharibi, huku mataifa mengine duniani yakiangalia kwa jicho la tahadhari, yakijiuliza: "Je, akiba zetu ziko salama Ulaya?"