Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, amefanya mkutano muhimu na viongozi wa Umoja wa Ulaya (EU) pamoja na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, hivi karibuni, kwa lengo la kuimarisha usalama wa Ukraine wakati huu wa vita na Urusi.
Katika mkutano huo, Macron alisisitiza haja ya kuundwa kwa kikosi cha pamoja cha EU ambacho kitasaidia Ukraine kuimarisha ulinzi katika miji yake muhimu. Alieleza kuwa kikosi hiki kitakuwa sehemu ya makubaliano yoyote ya amani yatakayofikiwa na kitatumika kukabiliana na mashambulizi yoyote kutoka kwa Urusi.
"Licha ya madai ya Urusi ya kutaka amani, wanaendelea na mashambulizi ya kila siku dhidi ya ngome za Ukraine, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya kiraia. Mashambulizi haya lazima yakome," alisema Macron.
Macron, kwa kushirikiana na Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, wamekuwa wakihamasisha kuundwa kwa muungano wa kimataifa ambao utaiwezesha Ukraine kupata msaada wa kijeshi kutoka EU. Juhudi hizi zimekuwa zikikumbana na changamoto kutokana na tofauti za maoni miongoni mwa nchi wanachama kuhusu aina ya msaada unaohitajika.
Hata hivyo, Macron na Starmer wanaendelea na juhudi zao za kuunda muungano imara wa kimataifa ili kuleta amani ya kudumu nchini Ukraine. Mkutano huu unaonyesha dhamira ya Ufaransa na washirika wake katika kuunga mkono Ukraine katika kipindi hiki kigumu.