Marekani imeonya kuwa inaweza kuweka vikwazo dhidi ya maofisa wa serikali na jeshi wa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kufuatia mzozo unaoendelea Mashariki mwa DRC, ambapo waasi wa M23 wameuteka mji wa Goma na kuendelea kusonga mbele katika maeneo mengine.
Kwa mujibu wa barua ya kidiplomasia iliyoonekana na shirika la habari la Reuters, Marekani inazitaka pande zote mbili kuchukua hatua za kurejesha utulivu kabla ya mkutano wa kilele wa kikanda uliopangwa kujadili mgogoro huo.
Mgogoro kati ya Rwanda na DRC umeendelea kuzua wasiwasi wa kimataifa, huku kila upande ukimlaumu mwenzake kwa kuchochea machafuko. DRC inaituhumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23, huku Rwanda ikidai kuwa DRC inatoa hifadhi kwa wapiganaji wa kundi la FDLR, linaloundwa na Wahutu waliokimbilia DRC baada ya mauaji ya kimbari ya 1994 nchini Rwanda.
Katika ujumbe wa kidiplomasia uliotumwa Ijumaa na Marekani kwenda Kenya, nchi ambayo inashikilia uenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na imekuwa mpatanishi katika mzozo huo, Washington ilisisitiza kuwa utulivu katika eneo hilo utategemea Rwanda kuondoa vikosi vyake na silaha zake kutoka DRC.
"Tunapoweka matakwa haya kwa pande zote mbili, tutazingatia uwezekano wa kuweka vikwazo dhidi ya wasio washirika, pamoja na maofisa wa jeshi na serikali katika serikali zote mbili," ilisema taarifa hiyo.
Hatua hii ya Marekani inakuja wakati juhudi za kidiplomasia zikiongezeka kutafuta suluhisho la mgogoro huo, huku jumuiya ya kimataifa ikiendelea kushinikiza pande zote mbili kuachana na mapigano na kutafuta suluhu ya amani.