Serikali ya Rwanda imetoa taarifa kali kulaani vikwazo vilivyowekwa na Marekani dhidi ya Waziri wake anayeshughulikia Muungano wa Kikanda, Jenerali Mstaafu James Kabarebe. Rwanda imeyataja vikwazo hivyo kuwa ni hatua zisizo na msingi wowote.
Marekani imemtuhumu Jenerali Kabarebe kwa kuhusika katika mgogoro unaoendelea Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), hasa kutokana na madai ya uhusiano wake na kundi la waasi la M23. Pamoja na Jenerali Kabarebe, Marekani pia imemwekea vikwazo msemaji wa M23, Lawrence Kanyuka. Hata hivyo, serikali ya Rwanda imesisitiza msimamo wake wa kukanusha vikali tuhuma zozote za kuunga mkono kundi hilo la waasi.
Msemaji wa Serikali ya Rwanda, Yolande Makolo, amesema kuwa hatua ya Marekani haina msingi na haikubaliki. Badala yake, ameihimiza jumuiya ya kimataifa kuunga mkono kikamilifu juhudi za kisiasa zinazoongozwa na mataifa ya kikanda katika kutafuta suluhu ya kudumu kwa mgogoro unaoikumba Mashariki mwa DRC kwa muda mrefu.
"Vikwazo hivi havitasaidia kuleta suluhu ya kweli kwa mgogoro wa muda mrefu Mashariki mwa DRC. Kama vikwazo vingekuwa na ufanisi, basi eneo hili lingekuwa na amani kwa muda mrefu sasa," alisema Bi. Makolo kwa masikitiko.
Marekani ilitangaza vikwazo hivyo jana, ikimtuhumu Jenerali Kabarebe kwa kuhusika na masuala ambayo yanazidi kuchochea hali ya sintofahamu na ukosefu wa utulivu katika ukanda huo wa Afrika Mashariki. Kwa sasa, Jenerali Kabarebe anahudumu kama Katibu wa Nchi katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Rwanda, ambapo anasimamia masuala yanayohusu ushirikiano wa kikanda.
Mgogoro wa Mashariki mwa DRC umekuwa chanzo kikuu cha mvutano kati ya Rwanda na DRC kwa muda mrefu. Mataifa ya kikanda, ikiwa ni pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), na jumuiya ya kimataifa kwa ujumla, zimekuwa zikihimiza pande zote mbili kufanya mazungumzo ya kisiasa kwa lengo la kupata suluhu ya kudumu na amani katika eneo hilo. Vikwazo hivi vya Marekani vinaweza kuongeza changamoto katika juhudi hizo za kidiplomasia.