Serikali ya Canada imetangaza vikwazo vya kiuchumi na kisiasa dhidi ya Rwanda, ikituhumu taifa hilo kwa kusaidia kundi la waasi la M23 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Tangazo hilo limekuja kufuatia ukosoaji wa Canada dhidi ya mashambulizi na mauaji yanayotekelezwa dhidi ya raia, wakimbizi, na vikosi vya Umoja wa Mataifa katika eneo la Mashariki mwa DRC.
Vikwazo vilivyowekwa na Canada vinajumuisha kusitisha huduma za teknolojia na ushirikiano wa kibiashara na Rwanda. Hatua hii ni sehemu ya juhudi za kimataifa za kushinikiza Kigali kusitisha uhusiano wake na waasi wa M23.
Rwanda, hata hivyo, imejibu vikali uamuzi huo, ikidai kuwa Canada inashindwa kutambua mashambulizi yanayotekelezwa dhidi ya raia wa kabila la Banyamulenge ndani ya DRC. Serikali ya Rwanda imesisitiza kuwa vikwazo hivyo havitasaidia kutatua mgogoro unaoendelea katika eneo hilo.
Hatua ya Canada inafuatia vikwazo vilivyowekwa na Ubelgiji, Uingereza, na Marekani dhidi ya Jenerali James Kabarebe wa Rwanda, ambaye anatuhumiwa kuhusika katika kuwasaidia waasi wa M23.
Rwanda imeendelea kukanusha madai ya kutuma wanajeshi wake nchini DRC, ikisisitiza kuwa juhudi zake zinalenga kulinda mipaka yake dhidi ya mashambulizi ya kundi la waasi la FDLR, ambalo lina uhusiano wa kihistoria na waliohusika katika mauaji ya kimbari ya 1994.
Hali hii inaashiria kuongezeka kwa mvutano wa kidiplomasia kati ya Rwanda na mataifa ya Magharibi, huku jumuiya ya kimataifa ikiendelea kushinikiza suluhisho la amani kwa mzozo wa Mashariki mwa DRC.