Kizaazaa Marekani: Mkwamo wa Serikali Wafuta Ndege 1000, Waongozaji (ATC) Wafanya Kazi Siku 39 Bila Mshahara

international | Sun Nov 09 2025


Kizaazaa Marekani: Mkwamo wa Serikali Wafuta Ndege 1000, Waongozaji (ATC) Wafanya Kazi Siku 39 Bila Mshahara

Hali ya usafiri wa anga nchini Marekani imeingia katika mgogoro mkubwa, huku zaidi ya safari 1,000 za ndege, za ndani na kimataifa, zikifutwa kwa siku ya pili mfululizo hii leo, Novemba 8. Kizaazaa hiki kinatokana moja kwa moja na "Mkwamo wa Serikali" (Government Shutdown) ambao sasa umetimiza siku 39, na kuweka rekodi ya kuwa mrefu zaidi katika historia ya taifa hilo.


Kiini cha tatizo hili ni uchovu na msongo wa mawazo unaowakabili waongozaji wa trafiki za angani (ATCs). Wafanyakazi hawa muhimu, ambao usalama wa mamilioni ya wasafiri uko mikononi mwao, wanalazimika kufanya kazi bila kulipwa mshahara tangu mkwamo huo uanze.


Kutokana na hali hiyo mbaya ya usalama, Shirika la Shirikisho la Anga la Marekani (FAA) limetangaza hatua za dharura. FAA imesema itapunguza uwezo wa kupokea na kuruhusu safari za ndege katika viwanja 40 vikubwa na vyenye shughuli nyingi zaidi nchini humo. Upunguzaji huo, ambao utafikia hadi asilimia 10, utatekelezwa kikamilifu ifikapo Novemba 14.


Mpango wa FAA ni kupunguza safari kwa awamu ili kudhibiti hali: ulianza kwa asilimia 4 jana (Novemba 7), utaongezeka hadi asilimia 6 ifikapo Novemba 11, kisha asilimia 8 (Novemba 13) na kufikia asilimia 10 (Novemba 14). Shirika hilo limesisitiza kuwa hatua hizi ni muhimu kwa ajili ya usalama wa anga, kwani waongozaji ndege wamechoka kutokana na kufanya kazi kupita kiasi bila malipo.


Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Newark Liberty huko New Jersey umeripotiwa kuwa mmoja ya iliyoathirika zaidi. Shirika la habari la CNN liliripoti kuwa kufikia jana mchana, safari za kuwasili zilikabiliwa na ucheleweshaji wa wastani wa zaidi ya saa nne, huku zile za kuondoka zikichelewa kwa saa moja na nusu.


Takwimu kutoka 'FlightAware' zinaonyesha kuwa viwanja vilivyoongoza kwa kufuta safari nyingi zaidi ni pamoja na Charlotte/Douglas, Newark Liberty, na Chicago O'Hare. Aidha, ucheleweshaji mkubwa umeripotiwa katika viwanja vingine muhimu kama John F. Kennedy (JFK) (takriban saa 3), Hartsfield-Jackson Atlanta (zaidi ya saa 2 na nusu), na LaGuardia (karibu saa 1).


Mgogoro huu umetokea katika wakati mbaya zaidi, kwani Marekani inakaribia msimu wa safari wenye shughuli nyingi zaidi mwaka mzima, kuelekea sikukuu kubwa ya "Shukrani" (Thanksgiving) mnamo Novemba 27. Hali hii inatabiriwa kuongeza adha na usumbufu mkubwa kwa mamilioni ya wasafiri.


Akizungumzia hali hiyo, Waziri wa Uchukuzi, Son Duffy, aliandika kwenye mtandao wa X (zamani Twitter) kwamba hata ndege za kibinafsi (private jets) hazitasalimika. Alisema serikali inatekeleza vikwazo maalum dhidi yao. "Tumepunguza safari za ndege za kibinafsi katika viwanja vyenye shughuli nyingi," alisema Duffy. "Tunawaelekeza kutumia viwanja vidogo ili kuruhusu waongozaji ndege waliozidiwa kuzingatia safari za kibiashara."


Tatizo si kwa waongozaji ndege pekee. Takriban wafanyakazi 64,000 wa Mamlaka ya Usalama wa Uchukuzi (TSA), wale wanaowakagua abiria na mizigo viwanjani, nao pia wanafanya kazi bila malipo. Vyama vya wafanyakazi vinaripoti kuwa wengi wa wafanyakazi hawa muhimu wameanza kuchukua likizo za ugonjwa au kutafuta kazi za pili ili kujikimu kimaisha.


Wakati wa mkwamo kama huu mwaka 2018 chini ya utawala wa Donald Trump, hadi asilimia 10 ya wafanyakazi wa TSA walichagua kubaki nyumbani badala ya kufanya kazi bila malipo.


Waziri Duffy ametoa onyo kali. Akiongea na kituo cha Fox News jana, alisema iwapo mkwamo huu wa serikali hautatatuliwa hivi karibuni, wizara yake italazimika kuongeza kiwango cha upunguzaji wa safari za ndege hadi kufikia asilimia 15 au hata 20.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.