Hali si shwari huko ughaibuni. Wakati dunia ikiendelea kushangilia kasi ya mabadiliko ya teknolojia, watafiti kutoka chuo kikuu chenye hadhi ya juu duniani, Taasisi ya Teknolojia ya Massachusetts (MIT), wamekuja na taarifa ambazo ni kama 'kaa la moto' kwa soko la ajira. Utafiti huo mpya unaonyesha kuwa Teknolojia ya Akili Mnemba (Artificial Intelligence - AI) imekomaa kiasi cha kuweza kuchukua nafasi za kazi kwa asilimia 11.7 ya nguvu kazi yote nchini Marekani.
Utafiti huu, uliofanywa kwa ushirikiano na Maabara ya Kitaifa ya Oak Ridge (ORNL) iliyo chini ya Wizara ya Nishati ya Marekani, umeweka wazi kuwa teknolojia hii siyo hadithi za 'abunuwasi' tena, bali ni uhalisia unaoishi nasi. Watafiti hao wametumia kipimo walichokipa jina la "Iceberg Index" au kwa Kiswahili tungeweza kusema 'Kipimo cha Mlima wa Barafu' kuchambua athari hizi.
Kile Tusichokiona Ndicho Hatari Zaidi
Kwa nini wameita 'Iceberg'? Watafiti wanasema kile tunachokiona kwa macho—kama vile roboti zinazofanya kazi viwandani au 'chatbots' zinazojibu maswali mtandaoni—ni ncha tu ya mlima wa barafu. Sehemu hii inayoonekana inachangia asilimia 2.2 tu ya thamani ya mishahara yote, ambayo ni sawa na Dola bilioni 211 (takriban Shilingi za Kitanzania Trilioni 569).
Hatari kubwa imejificha chini ya maji, sehemu ambayo haionekani kwa urahisi. Utafiti huo unabainisha kuwa kazi za 'kola nyeupe' kama vile Rasilimali Watu (HR), Lojistiki na Usafirishaji, Usimamizi wa Fedha, na kazi za kawaida za ofisini ndizo zipo kwenye hatari kubwa zaidi ya 'kuliwa kichwa' na AI. Thamani ya kazi hizi zilizojificha inafikia asilimia 11.7 ya jumla ya mishahara ya wafanyakazi wote Marekani, kiasi ambacho ni takriban Dola trilioni 1.2 (zaidi ya Shilingi za Kitanzania Trilioni 3,200).
Hakuna Pa Kukimbilia: Mjini na Vijijini
Kama ulidhani wimbi hili litapiga katika majiji makubwa pekee kama New York au California, umekosea. Ripoti hiyo inabainisha kuwa 'tsunami' hii ya AI haichagui mjini wala kijijini. Majimbo yote 50 ya Marekani yataathirika kwa namna moja au nyingine. Watafiti wanasisitiza kuwa vipimo vya kawaida vya uchumi kama Pato la Taifa (GDP) au takwimu za ukosefu wa ajira haviwezi kuona picha kamili ya mabadiliko haya yanayokuja kwa kasi ya mwanga.
"Tulitumia muda mwingi kujaribu kuifanya AI iwe na akili, lakini sasa changamoto kubwa ni kutabiri nini kitatokea pindi akili hiyo itakapoanza kufanya kazi na binadamu," walieleza watafiti hao. Wanafananisha soko la sasa la ajira na "jamii chotara" (hybrid society) ambapo wafanyakazi binadamu milioni 150 wanashirikiana na maelfu ya "mawakala wa AI" (AI agents).
Si Ramli, Bali ni Dira ya Kujipanga
Hata hivyo, wataalamu hao wametoa angalizo muhimu. Kipimo cha 'Iceberg Index' siyo ramli ya kutabiri kuwa kesho watu wataamka na kukuta hawana kazi. Badala yake, ni picha halisi (snapshot) inayoonyesha uwezo wa sasa wa teknolojia hiyo. Lengo ni kuwapa viongozi, watunga sera, na wamiliki wa makampuni taarifa sahihi ili waweze kufanya maamuzi magumu sasa.
Ujumbe mkubwa hapa ni juu ya umuhimu wa kuwekeza kwenye elimu na ujuzi mpya. Badala ya kusubiri mpaka maji yafike shingoni, makampuni yanashauriwa kuanza kuwapa wafanyakazi wao mafunzo yatakayowawezesha kufanya kazi sambamba na AI badala ya kushindana nayo.
Kwa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla, hii ni kengele ya kuamsha walio lala. Ingawa utafiti huu unahusu Marekani, historia inaonyesha kuwa kile kinachotokea katika uchumi mkubwa duniani hufika kwetu kama mafuriko. Ni wakati wa taasisi zetu za elimu na serikali kuanza kutafakari upya mitaala na sera zetu za ajira ili kizazi kijacho kisiweze 'kupigwa na butwaa' wakati teknolojia inapoamua kushika hatamu.