Dunia imepata mshtuko mpya wa kiuchumi baada ya Taasisi maarufu ya Teknolojia ya Massachusetts (MIT) kuweka hadharani utafiti unaotisha unaoonyesha jinsi Akili Mnemba (Artificial Intelligence - AI) inavyojipanga kufuta mamilioni ya ajira. Utafiti huo, uliofanywa kwa kushirikiana na Maabara ya Taifa ya Oak Ridge (ORNL), umebainisha kuwa asilimia 11.7 ya soko la ajira nchini Marekani lipo hatarini kupotea hivi sasa kutokana na teknolojia iliyopo.
Kwa lugha ya fedha, hii inamaanisha kuwa mishahara yenye thamani ya Dola trilioni 1.2—kiasi ambacho ni sawa na takriban Shilingi Trilioni 3,240 za Kitanzania—ipo hatarini kuyeyuka na kwenda kwa maroboti na programu za kompyuta. Hii ni bajeti ambayo inaweza kuendesha nchi nyingi za Afrika kwa karne nzima.
Siri ya 'Iceberg Index': Kilichojificha ni Kikubwa
Watafiti hao wametumia kipimo kipya walichokipa jina la ‘Iceberg Index’ au "Kipimo cha Barafu." Falsafa yake ni rahisi: Unapoona barafu baharini, kile kinachoonekana juu ni kidogo sana (ncha ya barafu), lakini kilichojificha chini ya maji ni kikubwa na cha hatari zaidi.
Ili kupata majibu haya, watafiti hawakupiga ramli; walitengeneza "mapacha wa kidijitali" (digital twins) wa wafanyakazi milioni 151 wa Marekani. Walichambua kila kitu kuwahusu—wanapoishi, kazi wanazofanya, na ujuzi walionao—kisha wakalinganisha na uwezo wa AI ya sasa.
Matokeo yameonyesha kuwa kelele tunazosikia kuhusu kufutwa kazi katika makampuni ya teknolojia (kama Google au Meta) ni sehemu ndogo sana, inayokadiriwa kuwa asilimia 2.2 tu ya mishahara yote (sawa na Shilingi Trilioni 570). "Janga la kimyakimya" liko kwenye zile kazi ambazo hatukudhani zingeguswa.
Sekta Zilizo Hatarini: Sio IT Tu!
Hapa ndipo penye mshangao. Kwa miaka mingi, tuliaminishwa kuwa AI itachukua kazi za viwandani au za kuandika kodi za kompyuta. Lakini utafiti huu wa MIT umepindua meza.
Sekta zilizo hatarini zaidi ni zile tunazoziona kama "salama", zikiwemo:
- Rasilimali Watu (HR): Kazi za kuajiri na kusimamia maslahi ya wafanyakazi.
- Usafirishaji na Lojistiki: Uratibu wa mizigo na stoo.
- Utawala na Ofisi: Makatibu muhtasi na wasaidizi wa ofisini.
- Fedha (Finance): Wahasibu na wachambuzi wa fedha.
Utafiti unasema, "Athari iliyojificha (chini ya barafu) ina thamani ya Dola trilioni 1.2." Hii ina maana kuwa kazi nyingi za ofisini ("White-collar jobs") ambazo Watanzania wengi wanasomea vyuo vikuu leo, zinaweza kufanywa na AI kwa ufanisi na gharama nafuu zaidi.
Funzo kwa Sera na Mipango
Lengo la Iceberg Index si kututisha ili tukate tamaa, bali ni kutupa tochi ya kumulika gizani. Ni zana ya kuwasaidia watunga sera kujua wapi pa kuelekeza nguvu.
Tayari majimbo ya Marekani yameanza kuchukua hatua. Jimbo la Tennessee limetumia data hizi kuandaa "Mpango kazi wa Nguvukazi ya AI," huku majimbo ya Utah na North Carolina yakitumia ripoti hii kubadili mitaala ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi. Wanataka kujua ni ujuzi gani utahitajika kesho ili watu wao wasiwe vibarua wa mashine.
Mwisho wa Dhana ya 'Silicon Valley'
Utafiti huu pia umevunja mwiko mmoja mkubwa: Kwamba hatari ya AI ipo kwenye majiji makubwa ya kiteknolojia kama San Francisco na New York pekee. Ukweli ni kwamba, wimbi hili halichagui mjini wala kijijini.
Athari zimeonekana kusambaa kote katika majimbo 50 ya Marekani, zikiathiri hadi maeneo ya vijijini ambako kazi za usimamizi wa ofisi na lojistiki ndizo uti wa mgongo wa ajira.
Kwa Tanzania, hii ni kengele ya hatari. Ikiwa taifa lenye nguvu kama Marekani linahaha kuokoa ajira zake, sisi tunajipangaje? Ni wazi kuwa mitaala yetu na mikakati ya kukuza uchumi lazima sasa iweke maanani nguvu ya "Barafu hii ya AI" kabla haijatugonga tukiwa tumelala.