Kilio cha Ajira: Akili Mnemba (AI) Yaanza 'Kutafuna' Vichwa, McKinsey na HP Watangaza Kufuta Kazi Maelfu ya Wafanyakazi

it | Sun Nov 30 2025


Kilio cha Ajira: Akili Mnemba (AI) Yaanza 'Kutafuna' Vichwa, McKinsey na HP Watangaza Kufuta Kazi Maelfu ya Wafanyakazi

Mvumo wa teknolojia ya Akili Mnemba (Artificial Intelligence - AI) umeanza kugeuka kuwa jinamizi kwa wafanyakazi duniani. Wakati wengi wakishangilia uwezo wa roboti kurahisisha kazi, upande wa pili wa shilingi umeanza kuonekana kwa uchungu, huku makampuni makubwa ya kimataifa yakianza "kufyeka" wafanyakazi ili kupunguza gharama na kuongeza faida kwa kutumia mashine. Wiki hii, dunia imeshuhudia vigogo wawili, McKinsey & Company na HP Inc., wakitangaza mipango ya kupunguza nguvukazi yao kwa kishindo.


McKinsey: Wakongwe Wanaoshika Shoka


Kampuni ya ushauri wa kibiashara yenye hadhi ya juu duniani, McKinsey, ambayo imedumu kwa takriban miaka 100, imeripotiwa kuanza mchakato wa kuwaondoa kazini wafanyakazi wake wa kitengo cha teknolojia. Kwa mujibu wa ripoti kutoka Bloomberg, kampuni hiyo wiki iliyopita ilifuta ajira za wataalamu 200 wa teknolojia duniani.


Hii ni ishara mbaya kwa sababu McKinsey inajulikana kwa kuwa na wafanyakazi zaidi ya 45,000 na washirika (partners) 3,000, lakini sasa imeanza kutathmini ni wapi roboti zinaweza kufanya kazi za binadamu. Katika taarifa yao, McKinsey wamesema, "AI inatupa fursa ambayo haijawahi kutokea... tunajitahidi kufanya kazi zetu kwa ufanisi zaidi." Kwa lugha nyepesi ya kiuchumi, "ufanisi" hapa unamaanisha mashine moja kufanya kazi za watu kumi kwa gharama nafuu.


Inadaiwa kuwa katika kipindi cha miaka miwili ijayo, McKinsey inapanga kufanya tathmini kali zaidi itakayopelekea wafanyakazi wengi zaidi kupoteza vibarua vyao, huku AI ikichukua nafasi zao katika uchambuzi wa data na uandaaji wa mikakati.


HP na Panga la Watu 6,000


Hali ni mbaya zaidi kwa upande wa watengenezaji wa kompyuta na 'printers' maarufu duniani, HP Inc. Kampuni hiyo imetangaza mkakati mpya na wa kutisha unaolenga kupunguza kati ya wafanyakazi 4,000 hadi 6,000 ifikapo mwaka 2028.


Mkurugenzi Mtendaji wa HP, Enrique Lores, ameweka wazi kuwa lengo lao ni kuokoa kiasi cha Dola Bilioni 1 (sawa na takriban Shilingi Trilioni 2.7 za Kitanzania) kila mwaka. Lores amesisitiza kuwa ili kampuni hiyo ibaki kwenye ushindani, lazima ianze kutumia AI katika maeneo muhimu kama ukuzaji wa bidhaa, huduma kwa wateja (customer support), mauzo, na hata viwandani.


"Hili ni jambo la lazima kulifanya ili kulinda uhai wa kampuni yetu," alisema Lores.


Mpango huu wa kupunguza wafanyakazi utagharimu kampuni kiasi cha Dola milioni 650 (takriban Shilingi Trilioni 1.75 za Kitanzania) kama gharama za marekebisho (restructuring costs). Ikumbukwe kuwa HP, ambayo kwa sasa ina wafanyakazi takriban 58,000, ilishawahi kupunguza watu wengine 6,000 miaka mitatu iliyopita, ikiokoa Dola bilioni 2.2 (takriban Shilingi Trilioni 5.9 za Kitanzania).


Licha ya HP kutangaza mapato ya Dola bilioni 14.6 (takriban Shilingi Trilioni 39.4) katika robo ya nne ya mwaka—ongezeko la asilimia 4.2—bado faida yao (margins) inabanwa na ushuru wa bidhaa na kupanda kwa bei za vipuri (memory chips), jambo linalowasukuma kukimbilia AI kama mwokozi wa gharama.


Accenture Nayo Yamo


Wimbi hili haliko kwa McKinsey na HP pekee. Mshindani mkubwa wa McKinsey, kampuni ya Accenture, mwezi uliopita ilitangaza sera mpya ya "Kazi kwa Roboti." Mkurugenzi wao, Julie Sweet, alisema wazi kuwa wanapunguza wafanyakazi ambao hawawezi kubadilika au kufundishwa upya (retrain) ili kuendana na kasi ya AI. Hii ina maana kuwa hata kama kampuni inapata faida, kama kazi yako inaweza kufanywa na 'software', kibarua chako kipo mashakani.


Funzo kwa Soko la Ajira Tanzania


Matukio haya yanatoa ujumbe mzito kwa soko la ajira nchini Tanzania. Wakati tunapiga hatua katika uchumi wa kidijitali, ni wazi kuwa kazi za 'kukariri' zipo hatarini. Vijana na wataalamu wanapaswa kuongeza ujuzi (upskilling) katika maeneo ambayo mashine haziwezi kufanya kwa urahisi, kama vile ubunifu wa hali ya juu, uongozi, na utatuzi wa matatizo magumu (complex problem solving).


Dunia inaelekea mahali ambapo "kufanya kazi kwa bidii" hakutoshi tena; inahitajika "kufanya kazi kwa akili" huku ukiitumia teknolojia badala ya kushindana nayo. Kama makampuni makubwa yenye historia ya miaka 100 yanaamua kubadilika, sisi ni nani tusistuke?

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.