Huko nchini Australia, serikali imeamua kufunga 'bomba' la burudani kwa watoto kwa mtindo wa "kama wai, wai". Katika kile kinachotajwa kama sheria kali zaidi ya udhibiti wa mitandao duniani, kuanzia wiki ijayo, milango ya mitandao ya kijamii itafungwa rasmi kwa watoto wote wenye umri chini ya miaka 16. Waziri wa Mawasiliano wa nchi hiyo, Anika Wells, ametangaza msimamo wa "kauzu" akitaka ripoti za kila mwezi kutoka kwa kampuni za mitandao zikionyesha idadi ya akaunti za watoto zilizofutwa.
Hatua hii siyo ya lelemama. Serikali ya Australia imeweka mezani faini ya kutisha ya Dola za Australia milioni 50 (sawa na takribani Shilingi za Kitanzania Bilioni 87.5) kwa kampuni yoyote itakayoshindwa kuchukua hatua stahiki za kuwaondoa watoto hao kuanzia tarehe 10 ya mwezi huu. Orodha ya mitandao iliyolengwa na 'panga' hili inajumuisha vigogo wote wanaopendwa na vijana: Facebook, Instagram, TikTok, Snapchat, Reddit, X (zamani Twitter), na jukwaa la 'live streaming' la Twitch ambalo limeongezwa kwenye orodha hiyo wiki mbili zilizopita.
Google na Meta Wanyoosha Mikono
Katika kutii amri hiyo bila shuruti, kampuni ya Google imetangaza kuwa kuanzia tarehe 10, itawatoa (log out) watoto wote chini ya miaka 16 kwenye mtandao wa YouTube. Hii ina maana kuwa watoto hao hawatakuwa na uwezo wa kumiliki akaunti, kutengeneza 'playlist', wala kupakia video. Google itatumia data zake za siri na ishara za kidijitali (digital signals) kubaini umri halisi wa mmiliki wa akaunti.
"Tumekuwa tukisema wazi kuwa sheria hii ya haraka inaweza kuleta mkanganyiko, lakini tutatii," ilisema taarifa ya Google, huku ikionyesha wasiwasi kuwa sheria hiyo inaweza isiwe suluhisho la kudumu la usalama mtandaoni.
Kwa upande wa Meta, kampuni mama ya Facebook, Instagram na Threads, wao wamekuja na teknolojia mpya. Kuanzia tarehe 4, wataanza kufuta akaunti zinazotiliwa shaka. Ili kuhakikisha hakuna mtu mzima anayeonewa, Meta itatumia huduma ya utambuzi wa umri inayoitwa 'Yoti'. Mtumiaji atalazimika kutuma kitambulisho cha serikali au kupiga picha ya video ya uso wake (video selfie) ili kuthibitisha kuwa yeye si mtoto.
Kamishna wa Usalama wa Mtandao (eSafety) Kazini
Kamishna wa Usalama wa Mtandao wa Australia (eSafety Commissioner) amepewa rungu la kusimamia zoezi hili. Waziri Wells amesema kuwa kuanzia tarehe 11, siku moja baada ya sheria kuanza, barua za moto zitatumwa kwa kampuni zote 10 zikitakiwa kutoa takwimu za watoto waliofungiwa.
"Tunajua zoezi hili linaweza kuchukua muda kukamilika kwa asilimia 100, lakini endapo tutabaini kuna ukaidi wa kimfumo, mahakama itafanya kazi yake na faini itapigwa kwa kiwango cha juu kabisa," alisisitiza Waziri Wells alipozungumza na Klabu ya Waandishi wa Habari nchini humo.
Vita ya Mahakamani na Mwelekeo wa Dunia
Hata hivyo, sheria hii haijapita bila upinzani. Kikundi cha kutetea haki za kidijitali cha *Digital Freedom Project* chenye makao yake jijini Sydney, kimepanga kwenda Mahakama Kuu kuweka pingamizi (injunction) ili kuzuia sheria hiyo isianze kutumika. Serikali imejibu mapigo ikisema iko tayari kwa "bifu" lolote la kisheria ili kulinda afya ya akili ya watoto wa Australia dhidi ya madhara ya mitandao.
Wimbi hili la udhibiti linaonekana kusambaa duniani kote. Nchi ya Malaysia imetangaza kufuata nyayo hizo ifikapo mwaka 2026, huku Umoja wa Ulaya (EU), Ufaransa, na New Zealand zikiwa katika hatua za awali za kuweka mipaka ya umri kwa watumizi wa mitandao ya kijamii. Hii ni kengele ya kuamsha hata kwa nchi za Afrika kama Tanzania, ambapo matumizi ya mitandao kwa watoto yameanza kushika kasi bila udhibiti maalum.