Mradi kabambe wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) unatarajiwa kuwa mkombozi kwa vijana zaidi ya 12,000 kutoka mikoa minne ya Tanzania: Geita, Kagera, Tabora, na Tanga. Mradi huu unalenga kuwawezesha vijana kiuchumi na kupunguza tatizo sugu la ajira, ambalo limekuwa changamoto kubwa kwa taifa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo wilayani Bukombe, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko, alisema EACOP si tu bomba la kusafirisha mafuta, bali ni fursa ya maendeleo kwa Watanzania wa kawaida. Alisema mradi huu umetoa ajira kwa kampuni zaidi ya 200 za Kitanzania, na mabilioni ya shilingi yanazunguka katika uchumi wa nchi, na kuwanufaisha wajasiriamali wadogo kama akina mama ntilie na bodaboda. Hadi sasa, serikali ya Tanzania imewekeza takriban Sh. Trilioni 1.125 katika mradi huu, ambao umefikia asilimia 65 ya ukamilifu na unatarajiwa kukamilika Julai 2026.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi wa EACOP, Godfrey Mponda, tangu mwaka 2024, vijana 170 wameajiriwa moja kwa moja na mradi huo. Zaidi ya hayo, vijana 110 wamepelekwa masomoni na 238 wanapatiwa ufadhili wa masomo ili waweze kupata ujuzi unaohitajika kwa ajili ya maendeleo ya baadaye ya nchi.
Meneja wa Uwajibikaji kwa Jamii wa EACOP, Clare Haule, alieleza kuwa mradi huu unakwenda sambamba na miradi mingine ya kijamii, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya maji, barabara, elimu, na afya. Aliongeza kuwa kampuni hiyo inatambua changamoto za vijana ikiwemo ukosefu wa ajira, mafunzo stadi, na mitaji. Hivyo, awamu ya kwanza ya mradi huu itawezesha wananchi kiuchumi katika mikoa minne iliyotajwa, kabla ya awamu ya pili kuanza katika mikoa mingine.
Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Patrobas Katambi, alisema mradi huu wa EACOP ni moja ya miradi ya kimkakati ya serikali inayotekelezwa kwa ushirikiano na wadau mbalimbali. Alisisitiza kuwa serikali imetunga sera na sheria za kusaidia vijana kupata mitaji na fursa za ajira, ili waweze kunufaika moja kwa moja na miradi mikubwa inayotekelezwa nchini.