Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kudhihirisha utekelezaji wake wa dhati wa Itifaki ya Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Hatua hizi zinachukuliwa kwa kuzingatia maslahi mapana ya watu wa Afrika Mashariki na kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi wa kanda nzima. Utekelezaji huu haufanywi tu kwa maneno, bali kwa vitendo, kama ilivyojitokeza katika changamoto ya hivi karibuni ya kibiashara.
Tukio la kuwekewa vikwazo vya kuingiza bidhaa za kilimo kutoka Tanzania na mataifa ya Malawi na Afrika Kusini, ambayo si wanachama wa EAC, lilikuwa fursa ya kipekee kwa Tanzania kuonesha namna inavyoheshimu na kutekeleza itifaki za kibiashara za kikanda na kimataifa. Baada ya vikwazo hivyo kuwekwa, Tanzania ilitoa msimamo wake bayana kuwa haina nia ya kuingia katika vita vya kibiashara. Badala yake, ilitoa muda mfupi kwa nchi hizo kujitafakari na kuondoa vizuizi hivyo kupitia njia za kidiplomasia.
Kitendo hiki cha kuchagua kwanza njia ya majadiliano na si hatua za haraka za kulipiza kisasi kwa kufunga milango ya soko lake, kimeifanya Tanzania kuonekana kama mshirika mwenye busara na anayeheshimu mikataba. Ingawa baadaye Tanzania ilichukua hatua ya kuweka marufuku ya kuingiza baadhi ya bidhaa kutoka nchi hizo, hatua hiyo ilikuja tu baada ya ombi la awali la kidiplomasia kukaidiwa. Hii ilikuwa njia ya kusisitiza umuhimu wa kanuni ya biashara yenye usawa, yaani "kutoa na kupokea". Mara tu baada ya Malawi na Afrika Kusini kuonesha nia ya kuondoa vizuizi walivyoweka, Tanzania haikusita kufuta marufuku yake, ikidhirisha dhamira yake ya kutanguliza mazungumzo na ushirikiano.
Tunapongeza ustadi na umaahiri uliooneshwa na Wizara ya Kilimo, chini ya uongozi wa Waziri Hussein Bashe, katika kusimamia suala hili tata. Wizara imefanikiwa kutetea maslahi ya wafanyabiashara wa Tanzania huku ikilinda heshima na weledi wa nchi katika medani za kimataifa za biashara. Mfumo huu wa kusimamia mambo kwa weledi umewezesha Tanzania kushinda katika "majaribu" hayo ya kibiashara.
Ni matumaini yetu kuwa Tanzania itaendelea kuwa mfano wa kuigwa katika kutekeleza si tu Itifaki ya Soko la Pamoja ya EAC, bali itifaki zote za kikanda na kimataifa zinazolenga kukuza biashara na maendeleo. Utekelezaji wa dhati wa itifaki za EAC unachochea maendeleo katika sekta mbalimbali muhimu kama kilimo, viwanda, na miundombinu, kwani unarahisisha mzunguko wa bidhaa, huduma, mitaji, na hata watu ndani ya kanda.
Zaidi ya hayo, Soko la Pamoja linaimarisha uwezo wa pamoja wa nchi za EAC kukabiliana na mbinu mbalimbali za kiuchumi kutoka kwa mataifa makubwa duniani. Hii ni kwa sababu katika umoja kuna nguvu, na utengano ni udhaifu. Tunaamini kwamba vikwazo vya kiuchumi, hasa katika mazao ya kilimo vilivyokuwa vikitokea ndani ya EAC miaka ya nyuma, havitatokea tena. Kinachohitajika sasa ni kuendelea mbele, kuimarisha sera, sheria, na kanuni za biashara ili kufikia masoko yetu kwa ufanisi na uhakika.
Ni dhahiri kuwa kuweka masoko wazi kwa kufuata taratibu zilizowekwa ni njia mojawapo ya kujenga uwezo wa kiuchumi kwa wajasiriamali wa Tanzania na wa EAC kwa ujumla. Uuzaji wa bidhaa mbalimbali ndani ya kanda unapanua fursa za biashara na kuongeza kipato.
Kwa dhati kabisa, tunaipongeza Serikali ya Tanzania kwa kusimamia ipasavyo taratibu za biashara na kuhakikisha soko linaheshimika na kuwa wazi kwa wafanyabiashara kutoka nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Ni vyema kwa viongozi wa nchi nyingine za EAC kuiga mfano huu mzuri wa Tanzania katika kusimamia soko la pamoja. Kwa kuweka milango ya soko lao wazi kwa wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya kanda (kwa kufuata taratibu), nchi zinakuza uchumi wa watu wake na kukuza ustawi wa kanda nzima. Tanzania inatengeneza njia ya kuigwa kwa vitendo.