Uhusiano wa kihistoria na kidugu kati ya Tanzania na Oman sasa umepata nguvu mpya katika Nyanja ya kiuchumi, kufuatia hatua ya kampuni ya Kitanzania ya PMM Tanzania Ltd kuonesha meli tatu zitakazofungua rasmi daraja la bahari kwa ajili ya biashara ya moja kwa moja baina ya mataifa haya mawili.
Hatua hii inatajwa kuwa chachu muhimu itakayorahisisha usafirishaji wa bidhaa na kukuza biashara, ikiwa ni utekelezaji wa jitihada za serikali za kuimarisha diplomasia ya uchumi na uchumi wa bluu. Kampuni ya PMM, ambayo inajihusisha na masuala ya usafirishaji na madini, imejipambanua kama mdau muhimu katika kufanikisha azma hii baada ya kuonyesha uwezo wake mbele ya ujumbe wa wafanyabiashara kutoka Chemba ya Biashara ya Oman.
Akizungumza jijini Dar es Salaam baada ya ujumbe huo kutembelea kampuni hiyo, Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki na Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Abdallah Kilima, alieleza kuwa upatikanaji wa usafiri wa uhakika ni msingi mkuu wa kukuza biashara. "Huwezi kukuza biashara bila kuwa na usafiri wa uhakika. PMM wameonyesha meli tatu ambazo ziko tayari kuanza kazi ya kusafirisha bidhaa kati ya Tanzania na Oman, jambo ambalo linaenda sambamba na matarajio ya serikali ya kuona biashara ikiongezeka," alisema Balozi Kilima.
Kwa upande wake, Mwenyekiti Mtendaji wa PMM Group, Dk. Judith Spendi, alisisitiza kuwa fursa hii ni kubwa kwa uchumi wa Tanzania. Alieleza kuwa meli hizo zitasafirisha makontena mengi ya bidhaa za Kitanzania kama vile nyama ya mbuzi, nyama ya ng'ombe, chumvi, mbogamboga, na maua moja kwa moja hadi Oman. "Hii ni nafasi ya dhahabu kwa wazalishaji wetu. Wakati tukipeleka bidhaa zetu, meli hizi zitarejea na bidhaa zinazohitajika nchini kama mafuta na vifaa vya ujenzi kutoka Oman, na hivyo kukuza biashara pande zote mbili," alifafanua Dk. Spendi.
Mmoja wa wafanyabiashara kutoka Oman, Salim Albusaidi, alithibitisha kuwepo kwa fursa nyingi nchini baada ya ziara yao ya siku tano. Alisema wamevutiwa na uwekezaji katika sekta za kilimo cha mboga na matunda, madini, utalii, uvuvi na usindikaji. "Tumeichagua Tanzania kwa sababu ya historia yetu nzuri na tunaamini katika mwelekeo wake. Tayari baadhi ya mikataba imesainiwa na tunatarajia kuona wawekezaji wengi zaidi wakija," alisema Albusaidi, huku akitoa wito kwa Watanzania nao kwenda kuwekeza nchini Oman.