Utafiti mpya uliofanywa na mradi wa Kilimo, Chakula na Lishe (FoodLAND), unaosimamiwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), umebainisha uwepo wa changamoto kubwa ya ulaji wa vyakula vyenye protini miongoni mwa wananchi wanaoishi vijijini nchini Tanzania. Utafiti huo umeonyesha kuwa kiwango cha ulaji wa protini vijijini ni chini ya asilimia 60 ikilinganishwa na kile kinachoonekana katika maeneo ya mijini.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam mnamo Machi 27, 2025, Mratibu wa mradi wa FoodLAND kutoka SUA, Profesa Susan Nchimbi, alifafanua kuwa matokeo haya yana athari mbaya kwa afya na lishe bora ya mama wajawazito, wanaonyonyesha, na watoto wadogo. Aliongeza kuwa mradi wa FoodLAND unafanya kazi kwa bidii kuboresha hali hii kwa kufanya tafiti mbalimbali na kutoa mapendekezo yanayolenga kuboresha lishe kwa ujumla.
Profesa Nchimbi alieleza kuwa mradi umefanya tafiti za kina kuchunguza tabia za ulaji katika mazingira tofauti, na matokeo yameonesha wazi pengo kubwa katika ulaji wa protini kati ya wakazi wa mijini na vijijini. Upungufu huu wa protini unahatarisha afya ya makundi hayo muhimu katika jamii.
Alisisitiza kuwa ni muhimu kwa jamii kufahamu matokeo ya tafiti zinazofanywa kupitia miradi mbalimbali kama FoodLAND ili kuweza kuchukua hatua za kuboresha maisha yao na kuchangia maendeleo ya taifa. "Mara nyingi tunakuwa busy na utekelezaji wa miradi, lakini tunakosa muda wa kutoa taarifa kuhusu kile ambacho tumefanya na mafanikio tuliyopata. Nimeona ni jukumu langu kutoa taarifa hii ili wananchi waweze kujua," alisema Profesa Nchimbi.
Naye Profesa Dismas Mwaseba, mtafiti mwingine katika mradi wa FoodLAND, alieleza kuwa mradi huo umekuwa ukitekelezwa kwa muda wa miaka minne na nusu sasa, ukishirikisha nchi mbalimbali za Afrika na Kaskazini mwa Afrika, zikiwemo Morocco, Tunisia, Ethiopia, Kenya, Uganda, na Tanzania. Lengo kuu la mradi huu ni kutafuta suluhu endelevu kwa changamoto zinazohusu kilimo, upatikanaji wa chakula bora, na lishe katika nchi zinazoshiriki.
Utafiti huu unaonyesha wazi kuwa kuna haja ya kuongeza juhudi za kuhakikisha wananchi wa vijijini wanapata elimu kuhusu umuhimu wa ulaji wa vyakula vyenye protini kama vile maharage, samaki, nyama, na mazao mengine yanayopatikana kwa urahisi katika maeneo yao. Pia, kuna umuhimu wa kuweka mikakati ya kuongeza upatikanaji na uwezo wa wananchi kumudu kununua vyakula hivyo ili kuboresha afya na lishe ya mama na mtoto, na hivyo kuchangia katika ustawi wa jamii na taifa kwa ujumla. Mradi wa FoodLAND unaendelea kufanya kazi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha mapendekezo yanayotokana na tafiti zao yanazaa matunda na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.