Wapenzi na mashabiki wa klabu ya Stand United, maarufu kama "Chama la Wana," wanajiandaa kwa tukio kubwa la kihistoria litakalotikisa mji wa Shinyanga. Mnamo Oktoba 4, mwaka huu, Uwanja wa CCM Kambarage utafurika shamra shamra za Tamasha la "Siku ya Wana," ambalo kilele chake kitakuwa ni utambulisho rasmi wa kikosi kipya cha timu hiyo kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi ya Championship.
Akizungumza na wanahabari leo, Septemba 25, 2025, Mwenyekiti wa Tamasha, Chrispin Kakwaya, alieleza kuwa siku hiyo itakuwa ni karamu ya aina yake kwa mashabiki. Shughuli zitaanza tangu asubuhi hadi saa 12 jioni, zikipambwa na matukio mbalimbali. Kutakuwa na mashindano ya mbio za baiskeli kwa wanaume na wanawake, pamoja na burudani kutoka kwa wasanii maarufu wa Kanda ya Ziwa na wenyeji wa Shinyanga.
Ili kuongeza hamasa, kutakuwa na mechi za utangulizi zitakazozikutanisha timu za kijamii, ikiwemo pambano la watani wa jadi kati ya Madereva wa Bajaji na Bodaboda, pamoja na mechi kati ya wafanyabiashara wa Soko Kuu na Soko la Majengo, na michezo mingine ya kusisimua.
Baada ya burudani hizo, macho na masikio yote yataelekezwa kwenye jukwaa kuu, ambapo wachezaji wapya waliosajiliwa kuvaa jezi ya Stand United watatambulishwa mmoja baada ya mwingine. Ili kuthibitisha ubora wa kikosi hicho, siku itahitimishwa kwa pambano la kirafiki kati ya Stand United na timu kubwa inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, jina la timu hiyo likiwa bado ni siri kubwa.
"Natoa wito kwa wakazi wote wa Shinyanga, mashabiki wa Stand United, taasisi na mashirika mbalimbali kujitokeza kwa wingi kuiunga mkono timu yao. Hii ni siku yetu," alisema Kakwaya. Msemaji wa klabu, Ramadhan Zorro, aliongeza kwa kujinadi, akiahidi kuwa tamasha hili litakuwa la kipekee na la aina yake, tofauti na yote yaliyowahi kufanywa na timu nyingine nchini.