Hapatoshi leo kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga wakati Fountain Gate FC itakaposhuka dimbani kucheza mechi ya 'kifo au uzima' dhidi ya Stand United, ikiwa ni nafasi yao ya mwisho kabisa ya kujinusuru kushuka daraja kutoka Ligi Kuu Tanzania Bara.
Fountain Gate imejikuta katika hatua hii ya mtoano wa mwisho baada ya kupoteza katika mchezo wa awali wa mchujo dhidi ya Tanzania Prisons kwa jumla ya mabao 4-2. Baada ya kipigo hicho, sasa wana dakika 180 za mwisho dhidi ya Stand United, iliyotoka Ligi ya Championship, kuamua hatma yao ya kubaki Ligi Kuu au la.
Licha ya maumivu ya kupoteza mechi iliyopita, Ofisa Habari wa Fountain Gate, Issa Mbuzi, amesema kikosi chao hakijakata tamaa na kipo tayari kwa mapambano.
"Tunapaswa kuinua vichwa vyetu juu kwa sababu mapambano bado yanaendelea. Tuna dakika 180 za kuibakisha timu Ligi Kuu. Tunaamini tutafanya vizuri kuanzia mchezo wa leo kabla ya kumalizia kazi nyumbani Jumatatu," alisema Mbuzi, akionyesha matumaini.
Kwa upande wa wenyeji, Stand United, wao wanaona hii kama fursa ya kihistoria ya kurejea kwenye Ligi Kuu. Kocha wao, Juma Masudi, amesema wamejiandaa kikamilifu huku wakimpa heshima mpinzani wao.
"Tumefanya kila kitu kinachotakiwa kujiandaa. Tunakwenda kwenye mchezo tukimheshimu mpinzani wetu kwa sababu yeye anatoka Ligi Kuu, lakini tuna matumaini ya kupata matokeo mazuri si tu leo, bali hata kwenye mchezo wa marudiano," alisema Masudi.
Mshindi wa jumla wa michezo hii miwili atapata fursa ya kucheza Ligi Kuu msimu ujao. Iwapo Stand United itashinda, itapanda daraja na kuishusha Fountain Gate. Iwapo Fountain Gate itashinda, itabaki Ligi Kuu na kuiacha Stand United kwenye Championship. Mechi ya marudiano itapigwa Jumatatu kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Manyara.