Katika harakati za mwisho za kuipa motisha timu ya Stand United kabla ya mchezo wake wa marudiano wa mchujo (Play Off), Mbunge wa Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi, ametimiza ahadi yake ya kuikabidhi timu hiyo Shilingi milioni 5, na kuongeza ahadi nyingine ya Shilingi milioni 10 endapo timu hiyo itaibuka na ushindi.
Timu hiyo ya Shinyanga, inayojulikana kama 'Chama la Wana', inakabiliwa na kibarua kigumu cha kupindua matokeo baada ya kufungwa mabao 3-1 na Fountain Gate katika mchezo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Kambarage, Shinyanga mnamo Julai 4.
Licha ya kipigo hicho, Katambi, ambaye pia ni Naibu Waziri, alikabidhi fedha hizo jana kwa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, akisema lengo ni kuendelea kuwajenga wachezaji kisaikolojia kabla ya mchezo wa marudiano utakaochezwa leo, Julai 8, huko Manyara.
"Niliumia sana tulipopoteza mchezo wa nyumbani, lakini hatukati tamaa. Nina imani timu yetu inakwenda kufanya maajabu ugenini na kupata ushindi wa kishindo utakaotupandisha Ligi Kuu. Hizi milioni tano ni za kutimiza ahadi yangu ya awali, na wakishinda leo, nitatoa milioni 10 nyingine," alisema Katambi, huku akiwaomba mashabiki wote kuiombea timu yao.
Akipokea fedha hizo, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, alimpongeza Mbunge Katambi na wadau wengine ambao wamechangia jumla ya Shilingi milioni 25 kwa ajili ya kuihamasisha timu hiyo.
"Timu ina kikosi kizuri, kupoteza mechi ya kwanza ilikuwa ni ajali kazini. Nimezungumza na wachezaji na wako tayari kwa mapambano. Tunakwenda kufanya maajabu," alisema Mtatiro.
Ushindi wowote wa jumla kwa Stand United utairejesha timu hiyo kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya miaka kadhaa, huku ukiipeleka Fountain Gate kwenye Ligi ya Championship.