Wakati Young Africans SC (Yanga) wakijivunia huduma ya Nahodha wa zamani wa Simba, Mohamed Hussein 'Zimbwe Jr', klabu ya Simba SC sasa inajivunia beki wake mpya, Antony Mligo, ambaye ameanza kuingia haraka katika nyoyo za mashabiki wa Msimbazi. Mligo amefichua siri ya mafanikio yake na uwezo wa kuziba pengo kubwa la Zimbwe Jr, akisema msingi wake ni kujituma mazoezini, kujiamini, na kufahamu vizuri lengo la ujio wake ndani ya klabu.
Mligo, aliyejiunga na Simba msimu huu akitokea Namungo FC, alizungumza kwa unyenyekevu, akiahidi mashabiki watafurahi zaidi siku za usoni. Amesisitiza kwamba kiwango kidogo alichokionyesha mpaka sasa ni asilimia chache tu ya uwezo wake halisi, kwani bado anazoea mazingira.
"Namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa mwanzo huu mzuri. Hizi ni asilimia chache sana ambazo nimezionesha, kuna mambo mazuri mengi yanakuja. Bado kuna ugeni, ninachezea timu kubwa yenye mashabiki wengi, hiyo bado kidogo inaleta shida," alisema Mligo.
Shukrani na Deni kwa Mashabiki
Beki huyo wa kushoto alielezea shukrani zake za dhati kwa wanachama na mashabiki wa Simba ambao wameonekana kumpa upendo na kumkubali licha ya kucheza kwa muda mfupi tu. "Nawashukuru mashabiki wamenikubali sana. Nina deni kubwa kwao kwa kuniamini kiasi hiki, wamenifanya niendelee kujiamini na kuipambania nembo ya klabu," aliongeza. Mashabiki wa Simba wameonekana kumkubali Mligo haraka na kuanza kumsahau Zimbwe Jr.
Usajili wa Mbindo Uliyoongozwa na Kocha wa Zamani
Mligo alisajiliwa kwa mbinde kufuatia shinikizo na ushawishi mkubwa wa kocha wa zamani wa Simba, Fadlu Davids. Ilidaiwa awali baadhi ya viongozi wa Simba walikataa kumsajili Mligo, na badala yake walimsajili Miraji Athumani. Hata hivyo, Fadlu alipinga usajili huo na kutishia kutoa fedha mwenyewe mfukoni kumsajili Mligo baada ya kuvutiwa sana na kiwango chake akiwa Namungo. Hatimaye, viongozi walifanikiwa kumnasa.
Licha ya kuondoka kwa ghafla kwa Fadlu, Mligo ameendelea kusimika nafasi yake chini ya kocha mpya, Dimitar Pantev, akionesha kiwango bora katika michezo yote sita ya mashindano. Amecheza mechi nne za Ligi ya Mabingwa Afrika (dhidi ya Gaborone United na Nsingizini Hotspurs) pamoja na michezo miwili ya Ligi Kuu Tanzania Bara (dhidi ya Fountain Gate na Namungo).
Simba inajiandaa kuikabili JKT Tanzania, na Mligo ameahidi kuendeleza moto wake.