Licha ya klabu ya Simba kupokea kichapo cha mabao 4-1 kutoka kwa Al Hilal Omdurman ya Sudan, Meneja Mkuu mpya wa Wekundu wa Msimbazi, Dimitar Pantev, amewatoa hofu mashabiki akisema matokeo hayo ya mchezo wa kirafiki hayana umuhimu kwake, bali amepata picha kamili ya jinsi ya kukijenga kikosi chake kuwa tishio.
Akizungumza baada ya mtanange huo uliopigwa juzi jioni katika dimba la Gymkhana jijini Dar es Salaam, Pantev, ambaye amesimamia mechi mbili tangu achukue mikoba ya Fadlu Davids, aliyeelekea Raja Casablanca, alifafanua kuwa lengo lake kuu lilikuwa ni kuangalia maelewano ya kimbinu na utayari wa wachezaji. Alisema anaamini katika kujenga timu inayocheza kwa nidhamu, ikishambulia na kulinda kama kitengo kimoja, na tayari ameona dalili njema za kufikia lengo hilo.
"Siwezi kubadilisha kila kitu ndani ya muda mfupi, lakini nimeona ari ya vijana na jinsi wanavyoelewa ninachotaka. Michezo hii miwili ya kirafiki ilikuwa ni maabara yangu ya kuona nani yuko tayari kupambania nembo ya Simba. Matokeo si kipaumbele kwa sasa, bali kujenga mfumo," alisema kocha huyo. "Tunahitaji timu inayoshambulia kwa mpangilio na kujilinda kwa pamoja. Nina imani kubwa kuwa kila kitu kitakaa sawa na tutakuwa timu ya kuogopwa."
Katika mchezo huo, mabao ya Al Hilal yalifungwa na Adama Coulibaly, Hajj Madiki, na Sunday Adetunji aliyefunga mawili, huku bao la kufutia machozi la Simba likifungwa na Elie Mpanzu. Matokeo haya ni kinyume na mchezo wa awali kati ya timu hizi uliochezwa katikati ya wiki, ambapo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Pantev alikiri kuwa anafanya kazi bila baadhi ya nyota wake muhimu waliojiunga na timu zao za taifa, lakini akasisitiza kuwa wachezaji waliobaki wanapata maandalizi ya kutosha kimwili na kiakili ili pindi wenzao watakaporejea, iwe rahisi kuwaunganisha kwenye mfumo mpya.
Wakati huohuo, kikosi cha Simba kinatarajiwa kusafiri siku ya Alhamisi kuelekea Eswatini kwa ajili ya mchezo wa mkondo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Nsingizini Hotspurs. Mchezo huo muhimu unatarajiwa kupigwa siku ya Jumapili, saa kumi jioni, katika Uwanja wa Somhlolo.