Wakati Klabu ya Azam FC ikifanya usajili mkubwa kwa kumchukua Kocha Mkuu, Florent Ibenge, kutoka Al Hilal ya Sudan – huku ikitarajiwa kuondoka na wachezaji wengine wanne kutoka klabu hiyo – Klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam nayo imeingia vitani. Miamba hiyo ya Msimbazi imeonesha nia thabiti ya kukibomoa kikosi hicho cha Al Hilal kwa kuhitaji saini ya beki hodari wa kushoto, Khadim Diaw, raia wa Senegal.
Taarifa za ndani kutoka Simba, pamoja na vyanzo vingine vya kuaminika, zinaeleza kuwa klabu hiyo imeingilia kati dili ambalo lilikuwa likifuatiliwa kwa ukaribu na klabu ya JS Kabylie ya Algeria, ambayo ndiyo ilikuwa ya kwanza kuonesha nia ya kumsajili Diaw. Viongozi wa Simba wameamua kuingia kinyang'anyiro hiki wakilenga kumpa msaada beki wao mahiri, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’. Tshabalala ameonekana kucheza mechi nyingi mfululizo, jambo lililomfanya kuchoka na kushindwa kuonesha kiwango chake bora katika baadhi ya michezo muhimu.
"Diaw anatafuta changamoto mpya kabisa na tayari ameiweka wazi Al Hilal kuwa hataendelea na mkataba msimu ujao. Rais wa klabu hiyo amempa baraka za kuondoka," chanzo kimoja kiliweka wazi. "JS Kabylie waliwasiliana na wakala wake, lakini hawajatuma ofa rasmi. Hivyo basi, Simba wameingia rasmi kwenye mbio za kutaka kumsajili mchezaji huyu," kiliongeza chanzo hicho. Khadim Diaw alionesha kiwango cha hali ya juu katika Ligi ya Mabingwa Afrika akiichezea Al Hilal, ambapo walifika hatua ya robo fainali kabla ya kutolewa na Al Ahly ya Misri kwa jumla ya mabao 5-0 (1-0 nchini Mauritania na 4-0 nchini Misri).
Simba inaonekana kudhamiria kuimarisha safu yake ya ulinzi kwa kiasi kikubwa msimu ujao. Mbali na kumsaka Diaw, tayari imeanza mazungumzo na Lusajo Mwaikenda wa Azam FC, ambaye anatakiwa kwenda kusaidiana na Shomari Kapombe upande wa beki wa kulia. Ingawa Kapombe amekuwa akitumika katika michezo mingi, umri unaonekana kuanza kumtupa mkono, hivyo uwepo wa mchezaji mwingine mahiri utasaidia kupunguza mzigo.
Wakati harakati hizi za usajili zikiendelea, Simba imempa mkataba wa miaka mitatu kiungo mchanga Morice Abraham, ambaye amekuwa akifanya mazoezi na timu hiyo kwa muda mrefu. Kocha Mkuu, Fadlu Davids, ameridhishwa sana na uwezo binafsi wa Morice, akisisitiza uwezo wake wa kucheza nafasi nyingi uwanjani, ikiwemo winga wa kulia, winga wa kushoto, namba 10, na namba nane. Mchezaji huyu alikuwa nahodha wa Timu ya Taifa ya Vijana chini ya umri wa miaka 20, ingawa sasa ameshazidi umri huo.
Viongozi wa Simba wamebadili msimamo wao wa awali wa kusajili wachezaji wachache. Sasa wanataka kufanya usajili wa nguvu, kwani wametambua kuwa baadhi ya wachezaji waliowategemea kubeba timu wamewaangusha, huku viwango vyao vikishuka kila kukicha. Azim Dewji, mfadhili wa zamani wa timu hiyo, amekiri kuwa walikosea katika usajili wa msimu uliopita, akibainisha kuwa baadhi ya wachezaji wa kigeni hawakuwa na msaada mkubwa. Ameahidi kuwa watahakikisha wanasajili wachezaji bora zaidi kuelekea msimu ujao. "Tutasajili, tutasajili wachezaji bora kulingana na matakwa ya timu. Moja ya vitu vilivyotuangusha ni usajili; baadhi hawakukidhi matakwa ya timu, wengine walikuwa bora, lakini viwango vyao vilikuwa vinashuka kila mchezo," alisema Dewji.