Mchezaji na kocha wa zamani wa Simba, Talib Hilal, ametoa mbinu muhimu ambazo zinaweza kuisaidia timu hiyo kuibuka na ushindi katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Al Masry. Mtanange huo unatarajiwa kupigwa kesho saa 1:00 usiku katika Uwanja wa New Suez nchini Misri.
Akizungumza kutoka Oman, ambako anaishi hivi sasa, Talib, ambaye aliichezea Simba mwishoni mwa miaka ya 1980 hadi mwanzoni mwa miaka ya 1990, amemshauri Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, kumuanzisha Leonel Ateba katika safu ya ushambuliaji na kumtaka Elie Mpanzu kupunguza kukaa na mpira kwa muda mrefu na kufanya vitu visivyo na tija.
Talib, ambaye alichangia kwa kiasi kikubwa Simba kuiondoa Zamalek ya Misri katika Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003, pia aliwataka mabeki wa Simba kuwa makini na kuepuka kufanya mambo mengi wakiwa katika eneo la hatari.
"Katika ushambuliaji, naamini Ateba anafaa kucheza mbele kwa sababu ushirikiano wake na viungo washambuliaji umekuwa mzuri sana hivi karibuni. Sidhani kama kocha atabadili kikosi chake; naamini atatumia kikosi kilekile alichokuwa akikipanga," alisema Talib.
Aliongeza: "Mpanzu ajaribu kutumia kasi yake na uwezo wake wa kukokota mpira, lakini apunguze vitu ambavyo havina faida, hasa ugenini ambako timu inahitaji zaidi matokeo au mabao. Asikae sana na mpira, wapinzani hawatamuacha, lakini ni mchezaji mzuri ambaye anaweza kuchangia ushindi wa Simba."
Talib, ambaye alicheza kama beki wa kati wakati wake, aliwaonya mabeki wa Simba dhidi ya kujiamini kupita kiasi, akisema tabia hiyo inaweza kuwagharimu.
"Mabeki wa Simba wacheze kwa kujiamini na kucheza mipira rahisi. Beki anatakiwa kurahisisha kazi yake, si kuifanya iwe ngumu. Ukiwa beki, hupaswi kujiamini kupita kiasi; kosa moja linaweza kusababisha madhara. Nataka mabeki wacheze kama Abdulrazack Hamza, hana mambo mengi, anajiamini na anacheza mipira rahisi," alisema.
Akizungumzia mchezo huo kwa ujumla, Talib alisema utakuwa mgumu, lakini Simba inaweza kushinda au kutoa sare ikiwa itacheza kama ilivyocheza kwenye mechi zilizopita. Alisifu mbinu za Fadlu anapocheza ugenini.
"Mechi ni ngumu, kama unavyojua, timu za Misri zinajua sana kutumia uwanja wao wa nyumbani. Hata hivyo, siku hizi timu za Afrika zimeimarika na zinajua mbinu za kutumia. Pia, Simba si mara ya kwanza kucheza nchini Misri. Najua mechi hii itakuwa ngumu, lakini naamini Simba inaweza kupata ushindi ugenini," alisema Talib.
Aidha, alisema Fadlu ana uzoefu wa soka la Afrika, hasa anapocheza ugenini, kama ilivyoonekana kwenye mechi za makundi.
Simba imeondoka Ismailia leo kuelekea mji wa Canal, ambako mchezo huo utapigwa kesho. Mechi ya marudiano itapigwa Aprili 9 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.