Man United Ni Mambo Moto Europa: Bilbao Wapigwa 3-0 Nusu Fainali

sports | Fri May 02 2025


Man United Ni Mambo Moto Europa: Bilbao Wapigwa 3-0 Nusu Fainali

Manchester United, maarufu kama Mashetani Wekundu, walionyesha sura tofauti kabisa katika michuano ya Klabu Bingwa Ulaya (Europa League) ikilinganishwa na wanavyosuasua katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL). Timu hiyo ilipata ushindi mnono wa mabao 3-0 ugenini dhidi ya Athletic Bilbao ya Hispania katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali ya Europa League msimu wa 2024-2025, uliopigwa kwenye dimba la Estadio de San Mamés huko Bilbao mnamo May 1.


Matokeo haya yanawapa Man United matumaini makubwa kuelekea mchezo wa marudiano utakaofanyika katika uwanja wao wa nyumbani, Old Trafford, tarehe 9 Mei. Ushindi huu unakuja wakati ambapo timu hiyo inapitia moja ya misimu mibovu zaidi katika historia yao kwenye EPL. Wakiwa wamecheza mechi 34, wameshinda 10 tu, sare 9 na kupoteza michezo 15, wakiwa wamejikusanyia alama 39 pekee na kushika nafasi ya 14 kwenye msimamo. Tayari wameweka rekodi mbaya ya kupoteza mechi nyingi zaidi na watamaliza msimu na alama chache zaidi katika historia yao ya EPL (rekodi ya awali ilikuwa alama 58).


Hata hivyo, kwenye anga za Europa League, Man United wamekuwa hawakamatiki. Tangu kuanza kwa hatua ya makundi, hawajapoteza mchezo hata mmoja. Walimaliza hatua ya makundi wakiwa na ushindi mara 5 na sare 3. Kwenye hatua ya mtoano, waliwatoa Real Sociedad (16 bora) na Olympique Lyonnais (robo fainali) bila kupoteza, na sasa wameanza nusu fainali kwa kuichapa Athletic Bilbao. Kwa ujumla, wamecheza mechi 13 mfululizo katika michuano hii bila kuonja kichapo.


Katika mchezo dhidi ya Bilbao, bao la kwanza lilifungwa na kiungo mkabaji Casemiro dakika ya 30. Beki Harry Maguire alipiga krosi safi kutoka upande wa kulia, kiungo Manuel Ugarte akaukwamisha mpira kwa kichwa kumfikia Casemiro ambaye pia alitumia kichwa kuujaza wavuni.


Bahati ilikuwa upande wa Man United dakika ya 35 wakati beki wa Bilbao, Daniel Vivian, alipomchezea madhambi mshambuliaji Rasmus Højlund ndani ya eneo la hatari. Mwamuzi hakusita kumuonyesha Vivian kadi nyekundu ya moja kwa moja. Nahodha Bruno Fernandes alikwamisha penalti iliyotokana na faulo hiyo dakika ya 37, na kuifanya Man United kuongoza 2-0.


Wakicheza pungufu, Bilbao walijikuta wakizidiwa nguvu. Man United walitumia faida hiyo kuongeza bao la tatu dakika ya 45. Manuel Ugarte alionyesha ufundi kwa kutoa pasi ya kisigino iliyomkuta Bruno Fernandes, ambaye kwa ustadi aliuchipu mpira juu ya kipa na kufunga bao lake la pili na la tatu kwa timu yake.


Akizungumza baada ya mchezo, nahodha Bruno Fernandes, aliyefunga mabao mawili, alisema: "Ushindi huu ni muhimu sana. Dakika 20 za kwanza zilikuwa ngumu lakini mashabiki wetu hawakuacha kutushangilia. Napenda kufunga mabao na kutoa pasi za mabao, hiyo ni sehemu ya uwezo wangu." Aliongeza kuwa wanahitaji kuwa makini kwenye mchezo wa marudiano Old Trafford kwa sababu Athletic Bilbao ni timu nzuri, lakini anaamini kwa nguvu ya mashabiki wao nyumbani, watafanya vizuri. Ushindi huu unawapa nafuu kubwa Mashetani Wekundu na matumaini ya kumaliza msimu na angalau kombe moja muhimu.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.