Kufuzu WAFCON 2026: Shime Atamba Kuanza na Kishindo Chamazi, Ethiopia Yaja na Tahadhari

sports | Tue Oct 21 2025


Kufuzu WAFCON 2026: Shime Atamba Kuanza na Kishindo Chamazi, Ethiopia Yaja na Tahadhari

Macho na masikio ya mashabiki wa soka nchini Tanzania yatakuwa yameelekezwa katika Uwanja wa Azam Complex, maarufu kama Chamazi, jijini Dar es Salaam, kesho majira ya saa kumi na moja jioni. Hii ni wakati ambapo timu ya Taifa ya Wanawake, Twiga Stars, itakapoanza rasmi safari yake ya kumsaka mwali kuelekea Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) za mwaka 2026, kwa kuwakabili wapinzani wao kutoka Ethiopia.


Akizungumza na waandishi wa habari leo kuelezea maandalizi ya mchezo huo muhimu wa mchujo, Kocha Mkuu wa Twiga Stars, Bakari Shime, ameweka wazi kuwa kikosi chake kimekamilisha maandalizi na kiko tayari kwa vita ya kusaka ushindi mnono nyumbani.


Shime alithibitisha kuwa atalazimika kufanya mabadiliko kidogo kwenye mipango yake ya ufundi, kwani atamkosa mchezaji wake muhimu, Winfrida Gerald. Mchezaji huyo hataruhusiwa kucheza mchezo huo kutokana na kutumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoipata katika michezo iliyopita. Hata hivyo, kocha huyo alisisitiza kuwa pengo hilo litazibwa na halitakuwa kikwazo kwao.


Lengo kuu la Twiga Stars ni kuhakikisha wanapata tiketi ya kushiriki fainali hizo zitakazofanyika nchini Morocco. Ili kufanikisha hilo, Shime amesema ushindi katika mchezo wa kesho ni wa lazima ili kujiweka katika nafasi nzuri kabla ya mchezo wa marudiano.


"Huu ni mchezo muhimu sana kwetu," alisema Shime. "Ninaamini wachezaji wangu wameelewa vyema maelekezo niliyowapa. Watayaingia uwanjani wakiwa na nidhamu ya mchezo ili tuweze kupata matokeo mazuri tukiwa katika ardhi ya nyumbani."


Kocha huyo alienda mbali zaidi na kusema kuwa anaamini kikosi chake kiko juu kiwango na ubora kuliko wapinzani wao, na anatarajia Waethiopia watacheza kwa kujihami wakifahamu hilo. Hivyo, ametoa wito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi kuwapa sapoti.


"Malengo yangu ni kuendeleza historia nzuri kwa kuifunga Ethiopia. Nawaomba Watanzania waje kwa wingi Chamazi, uwepo wao utawapa nguvu wachezaji na kuwavunja moyo wapinzani," aliongeza.


Kuhusu hali ya kambi, Shime alithibitisha kuwa morali iko juu na hakuna majeruhi yeyote, isipokuwa mchezaji mmoja anayetumikia adhabu. Pia, alihakikisha kuwa wachezaji wote wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi (professionals) wameshawasili kambini na wamejiunga na wenzao kwa ajili ya maandalizi ya mwisho.


Kauli ya matumaini ilisisitizwa pia na Nahodha wa timu hiyo, Anastazia Katunzi. Kwa niaba ya wachezaji wenzake, Katunzi alisema wako tayari kupambana na kwamba wanafahamu uzito wa mchezo huo kwa Taifa.


"Sisi kama wachezaji tuko tayari kuvaana na Ethiopia. Tunatambua huu ni mchezo muhimu sana kwetu. Tumejipanga kufuata maelekezo yote ya mwalimu wetu ili tuweze kuwapa burudani na furaha Watanzania watakaojitokeza uwanjani," alisema Nahodha Katunzi.


Wakati Twiga Stars wakitamba, Kocha Mkuu wa Ethiopia, Yosef Gebrewold, yeye amesema anaingia kwenye mchezo huo kwa tahadhari kubwa. Gebrewold alikiri kuwa anatambua ubora wa Twiga Stars na kwamba ni miongoni mwa timu bora katika ukanda huu.


"Kwa upande wetu tumejiandaa vizuri kukutana na Twiga Stars. Tunafahamu ni timu bora na watakuwa na faida ya mashabiki wengi watakaowashangilia. Hilo halitutishi, tutapambana kwa nguvu zote kuhakikisha tunapata matokeo chanya tukiwa ugenini," alisema Gebrewold.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.