Katika kile kinachoweza kutajwa kama "kunusurika tundu la sindano", Philipo Kasanda, mwanafunzi wa Kidato cha Pili katika Shule ya Sekondari Kakola mkoani Shinyanga, amevuta hewa ya uhuru baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kufuta kesi nzito iliyokuwa ikimkabili yeye na wenzake tisa. Kijana huyo ambaye alijikuta akiwa mahabusu wakati wenzake wakiwa kwenye vyumba vya mitihani, ameoja ladha ya uhuru katika Mahakama ya Wilaya ya Kahama, huku akibubujikwa na machozi ya furaha iliyochanganyika na hofu ya mustakabali wa masomo yake.
Tukio hili la aina yake limejiri leo mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Mhe. Mwanaidi Mtemi, ambapo upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Jukael Jairo, uliwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na shauri hilo (Nolle Prosequi).
DPP Afuta Mashtaka Matano Mazito Wakili Jairo aliiambia mahakama kuwa DPP ameamua kuliondoa shauri la Jinai Namba 26543 la mwaka huu chini ya kifungu cha 92(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai. Washtakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na mashtaka matano mazito yaliyotokana na vurugu za baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025. Mashtaka hayo ni pamoja na kuchoma moto majengo, uharibifu wa mali za umma, na unyang'anyi wa kutumia silaha—makosa ambayo kisheria yana adhabu kali ikiwemo kifungo cha muda mrefu jela.
Mbali na mwanafunzi Philipo Kasanda, wengine walioionja "Neema ya Rais" na kuachiwa huru ni John Maduka, Issa Miraji, Emmanuel Magina, Charles Costantine, na Jumanne Mathias. Orodha hiyo pia inawajumuisha Anania Lazaro, Juma Bundu, na Peter Mirombo. Wote kwa pamoja wametoka mahabusu na kurejea uraiani kuungana na familia zao.
Ndoto Iliyotikiswa: Kilio cha Mtihani wa Taifa Licha ya furaha ya kuachiwa huru, mwanafunzi Philipo Kasanda anakabiliwa na mtihani mwingine wa kimaisha. Akizungumza kwa uchungu nje ya viunga vya mahakama, Philipo ameeleza jinsi kukamatwa kwake Novemba 4, 2025, kulivyomgharimu elimu yake. Kijana huyo ameshindwa kufanya Mtihani wa Upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili (FTNA), ambao ndio tiketi pekee ya kumwezesha kuingia Kidato cha Tatu.
"Namshukuru Mungu na Serikali kwa kunifutia kesi hii, giza lilikuwa limetanda mbele yangu. Lakini nina ombi moja; nisaidieni nirudi shule. Tangu nikamatwe, wenzangu wameshafanya mtihani wa Taifa ambao mimi nimeukosa. Matarajio yangu ni kwenda kuzungumza na wazazi wangu ili watafute utaratibu utakaoniwezesha kurudia mwaka au kufanya mtihani maalum ili nisisitishe ndoto zangu za elimu," alieleza Philipo kwa sauti ya chini yenye kuomba msaada.
Kilio cha Philipo kinagusa hisia za wengi, ikizingatiwa kuwa mfumo wa elimu nchini unamtaka mwanafunzi kufaulu upimaji wa Kidato cha Pili ili kuendelea na masomo. Kukosa mtihani huo kunamuweka katika njia panda ya kurejea darasani mwakani.
Wakili wa Utetezi: "Haki Imetendeka" Kwa upande wake, Wakili wa Utetezi aliyekuwa akiwapigania watuhumiwa hao, Bw. Evodius Rwamgobe, amepokea uamuzi huo kwa mikono miwili. Amesema kuwa upande wa utetezi hauna kipingamizi na hatua ya DPP, kwani imewanusuru wateja wake na adhabu ambayo ingeharibu maisha yao, hususan kwa mwanafunzi huyo mdogo.
"Hii ni hatua ya busara sana. Wateja wangu tisa wamesamehewa na sasa wako huru. Tunashukuru vyombo vya sheria kwa kuona mbali na kutoa nafasi ya pili kwa vijana hawa," alisema Rwamgobe.
Kuachiwa kwa kundi hili la Kahama ni mwendelezo wa utekelezaji wa maagizo ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kuwataka vijana walioingia kwenye mkumbo wa vurugu za uchaguzi kusamehewa ili kurejesha umoja wa kitaifa na kulinda nguvukazi ya taifa.