Nyuso za hofu na mashaka zimegeuka kuwa vifijo na nderemo katika kumbi za Mahakama kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Mwanza, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kutekeleza kwa vitendo agizo la Rais Dk. Samia Suluhu Hassan la kuwafutia mashtaka vijana waliotiwa mbaroni kwa makosa mazito ya uhaini na uharibifu wa mali wakati wa vurugu za Uchaguzi Mkuu.
Katika kile kinachotajwa kama "mkono wa huruma wa mama", jumla ya washtakiwa 210 wamevuta hewa ya uhuru leo, Novemba 24, 2025, baada ya upande wa Jamhuri kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na mashauri hayo (Nolle Prosequi). Hatua hii imekuja siku chache tu tangu Rais Samia, akizindua Bunge la 13 jijini Dodoma Novemba 14, 2025, atoe maelekezo mahususi kwa vyombo vya haki kutoa msamaha kwa vijana walioingia kwenye mkumbo wa kisiasa bila kudhamiria kufanya uhalifu.
Mwanza: Kanda ya Ziwa Yafuta Machozi Jijini Mwanza, ambako ndiko kulikuwa na idadi kubwa ya washtakiwa, jumla ya vijana 139 wameachiwa huru na kurejea uraiani kuungana na familia zao. Vijana hawa walikuwa wakikabiliwa na rundo la mashtaka mazito yakiwemo uhaini, kuchoma moto majengo ya serikali, uharibifu wa miundombinu na unyang'anyi wa kutumia silaha—matukio yaliyotokea wakati wa joto la matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 29.
Katika mgawanyo wa walioachiwa Mwanza; Mahakama ya Wilaya ya Ilemela imewaachia huru washtakiwa 76 waliokuwa wakikabiliwa na kosa la uhaini, wakati wenzao 63 waliokuwa katika Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana wakikabiliwa na kesi za uharibifu na uchomaji moto, nao wameonja ladha ya uhuru. DPP ameondoa kesi hizo kwa kutumia mamlaka yake kisheria, huku akiwaasa vijana hao kuwa raia wema.
Dar es Salaam na Arusha: Uhuru Warejea Hali kadhalika katika Jiji la Biashara la Dar es Salaam, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshuhudia kuachiwa kwa washtakiwa 47. Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swallo, Wakili wa Serikali Mkuu, Job Mrema akisaidiana na Cathbert Mbiling'i, walieleza kuwa DPP hana nia ya kuendelea na kesi hiyo dhidi ya washtakiwa hao waliokuwa wakikabiliwa na tuhuma za kula njama na kutenda uhaini.
Wakili Mrema alibainisha kuwa uamuzi huo umefanyika chini ya kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), Sura ya 20 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2023, kifungu ambacho kinampa DPP mamlaka ya kusitisha mashitaka wakati wowote kabla ya hukumu. Hata hivyo, mshtakiwa mmoja kati ya 48 bado amesalia kizimbani kuendelea na shauri lake kutokana na sababu za kisheria.
Kule jijini Arusha, Kanda ya Kaskazini, Hakimu Mkazi Mfawidhi Erasto Philly naye amewaachia huru washtakiwa 24 waliokuwa wakikabiliwa na makosa mawili mazito ya kula njama na uhaini, baada ya mawakili wa serikali kuwasilisha ombi la kufuta kesi hizo.
Utekelezaji wa Maagizo ya 'Daktari wa Maridhiano' Wachambuzi wa masuala ya sheria na siasa wameeleza kuwa hatua hii ni uthibitisho wa dhati wa Rais Samia katika kujenga taifa lenye umoja na mshikamano (4R's - Reconciliation). Katika hotuba yake bungeni, Rais alisisitiza: "Kwa wale ambao wanaonekana walifuata mkumbo na hawakudhamiria kufanya uhalifu, wawafutie makosa yao."
Kauli hii imepokelewa kama "maji jangwani" kwa familia za vijana hao, ambao wengi wao walikuwa wamekabiliwa na hatari ya adhabu kali, ikizingatiwa kuwa kosa la uhaini ni moja ya makosa yenye uzito wa juu zaidi katika sheria za nchi. Uhuru huu unatajwa kuwa ni deni kwa vijana hao kuwa mabalozi wa amani na kuepuka kutumika katika vurugu za kisiasa siku za usoni.