Tundu Lissu Ang'olewa Kucha Mahakama Kuu, Maombi Yake Dhidi ya Kesi ya Uchochezi Yakataliwa

politics | Fri Jul 11 2025


Tundu Lissu Ang'olewa Kucha Mahakama Kuu, Maombi Yake Dhidi ya Kesi ya Uchochezi Yakataliwa

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ya Dar es Salaam, imetupilia mbali maombi ya mapitio ya kisheria yaliyowasilishwa na Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, akipinga mwenendo wa kesi yake ya msingi inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Uamuzi huo umetolewa kwa sababu maombi hayo yaliwasilishwa kinyume cha taratibu za kisheria.


Katika maombi yake, Lissu alitaka Mahakama Kuu iitishe jalada la kesi yake kutoka Mahakama ya Kisutu ili ipitie na kutengua uamuzi wa mahakama hiyo wa Juni 2, 2025, wa kuahirisha kesi. Lissu alidai kuwa hakimu aliahirisha kesi bila sababu za msingi, isipokuwa tu kwa sababu upande wa Jamhuri ulikuwa umeomba baadhi ya mashahidi wao wahifadhiwe majina yao.


Hata hivyo, jopo la mawakili wa Serikali, likiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali Nassoro Katuga, liliweka pingamizi tatu, likisema maombi ya Lissu yalikuwa na upungufu wa kisheria.


Akitoa uamuzi mdogo jana, Jaji Elizabeth Mkwizu alisema amekubaliana na hoja za upande wa Jamhuri. Alifafanua kuwa kwa mujibu wa Kifungu cha 372 (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), amri ya mahakama ambayo haiihitimishi kesi (kama vile amri ya kuahirisha shauri) haiwezi kukatiwa rufaa wala kufanyiwa mapitio.


"Mleta maombi anapinga amri ya ahirisho la Juni 2, 2025. Kifungu cha 372 (2) cha CPA kinasema wazi kuwa amri ambayo haiitimishi shauri la msingi haiwezi kufanyiwa mapitio," alisema Jaji Mkwizu. "Kwa hiyo, nakubaliana na upande wa Jamhuri kwamba maombi haya yameletwa kinyume na sheria na ninayatupilia mbali."


Licha ya kutupilia mbali maombi hayo, Jaji Mkwizu alimweleza Lissu kuwa anaweza kuwasilisha upya maombi yake endapo atafuata taratibu sahihi za kisheria.


Katika kesi yake ya msingi katika Mahakama ya Kisutu, Tundu Lissu anakabiliwa na mashtaka ya kuchapisha taarifa za uongo kupitia mtandao wa YouTube. Anadaiwa kuchapisha maneno yaliyosomeka, 'Uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka jana, wagombea wa Chadema walienguliwa kwa maelekezo ya Rais' na kwamba 'Majaji ni Ma-CCM hawawezi kutenda haki'.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.