Kwa kuongozwa na msemo wa "Tahadhari Kabla ya Hatari," Wizara ya Maji, ikishirikiana na Chemba ya Migodi Tanzania (TCM), imeandaa mafunzo maalum ya siku tatu yatakayowakutanisha wataalamu kutoka sekta ya umma na binafsi. Lengo kuu ni kujadili na kuweka mikakati thabiti ya kuhakikisha usalama wa mabwawa ya majisafi na yale ya kuhifadhia tope lenye sumu kutoka migodini (Tailings Storage Facilities - TSF).
Mafunzo hayo muhimu yamepangwa kufanyika jijini Mwanza kuanzia Novemba 19 hadi 21, 2025, yakiwa na kaulimbiu, ‘Tahadhari za Dharura za Kukabiliana na Majanga ya Mabwawa ya Maji na Tope Sumu’.
Akizungumza na wanahabari jijini Dodoma, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Diana Kimario, alisema haya ni mafunzo ya tatu kufanyika mfululizo, yakionyesha dhamira ya serikali ya kutoa kipaumbele kwa suala la usalama wa mabwawa. Alisema mafunzo hayo yamekuwa na mchango chanya katika kujenga uelewa na kuleta wataalamu wa kimataifa nchini ili kubadilishana uzoefu.
"Serikali, chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, inaamini katika ushirikishwaji wa sekta binafsi. Ushirikiano huu na Chemba ya Migodi ni uthibitisho wa hilo. Tutaendelea kufanya kazi pamoja ili kuhakikisha sekta zetu za maji na madini zinaendeshwa kwa usalama na tija," alisema Kimario.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Chemba ya Migodi Tanzania, Benjamin Mchwampaka, aliipongeza serikali kwa kuandaa jukwaa hili muhimu, akisema linasaidia kujenga uwezo wa wataalamu wa ndani na kuhakikisha sekta ya madini inazingatia viwango vya juu vya usalama katika utunzaji wa mazingira.
Wizara imetoa wito kwa wadau wote wa mabwawa, wakiwemo wamiliki wa migodi, wahandisi, na wasimamizi kutoka ndani na nje ya nchi, kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kushiriki katika mafunzo hayo muhimu yatakayofanyika jijini Mwanza.