Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira nchini, Mhandisi Hamisi Kamando, amewataka wakaguzi wa migodi ya madini na baruti kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa, kuongeza ufanisi katika utendaji wao, na kuzingatia kikamilifu taratibu na sheria za nchi wakati wa kutoa huduma. Wito huu umetolewa Mei 29, 2025, jijini Mwanza, alipokuwa akifunga kikao kazi cha siku mbili kilichowakutanisha wakaguzi hao. Kikao hicho kililenga kuwajengea uwezo, ikiwa ni pamoja na kufanya maboresho ya kanuni mbalimbali zinazoongoza sekta ya madini na Sheria ya Baruti.
Mhandisi Kamando alisisitiza umuhimu wa wakaguzi kutokubali kuyumbishwa au kupotoshwa na mtu yeyote, na badala yake, waendelee kusimamia misingi ya kazi, weledi, na maadili mema. Aliongeza kuwa ni muhimu kuepuka vitendo vya rushwa na kushinda vishawishi vyote vinavyoweza kuathiri utendaji wao. "Natoa rai, tunatakiwa kuwajibika kwa kuzingatia nidhamu, uaminifu, uwazi na kuongeza bidii kwenye kazi ili kuhakikisha kuwa Sekta ya Madini inaendelea kuwa na mchango mkubwa kwenye Pato la Taifa," alisema Mhandisi Kamando.
Aidha, Mhandisi Kamando alifahamisha kuwa kikao hicho kimefikia mapendekezo muhimu ya kufanya maboresho kwenye Kanuni za Usalama, Afya, na Utunzaji wa Mazingira katika migodi. Alieleza kuwa kanuni zilizopo zimepitwa na wakati, hasa ikizingatiwa kuwa Sheria ya Madini Sura ya 123 ilifanyiwa marekebisho makubwa mwaka 2017, lakini kanuni zake hazijasasishwa hadi sasa. "Kutokana na marekebisho ya Sheria ya Madini ni vyema sasa tukafanya maboresho ya kanuni za usalama, afya na mazingira ili ziweze kwenda sambamba na Sheria na hivyo, kuimarisha ufanisi wa kazi," alieleza.
Mbali na hilo, Mhandisi Kamando aligusia kuhusu Sheria ya Baruti ya mwaka 1963 na kanuni zake za mwaka 1964, akisema kuwa nao wameona ni muhimu kufanyia maboresho ili usimamizi wa matumizi ya baruti nchini uweze kuwa bora zaidi na salama.
Naye Mwanasheria Mwandamizi wa Tume ya Madini, Damian Kaseko, alipowasilisha mapendekezo kuhusu Sheria ya Baruti, Sura ya 45, alieleza kuwa maboresho yanayopendekezwa yanalenga kuboresha vifungu mbalimbali vya sheria hiyo ili kuleta ufanisi zaidi katika usimamizi wa utekelezaji wake. Sheria hii ilitungwa miaka mingi iliyopita (1963), hivyo kuna haja ya kuilinganisha na hali ya sasa.
Kwa upande wake, Siri Boga, akizungumza kwa niaba ya washiriki wa kikao kazi, alisema kuwa kikao hicho kimekuwa cha manufaa makubwa kwa wakaguzi wa madini kwani wamejengewa uwezo na kupatiwa mbinu mpya za kisasa wanazopaswa kuzifuata wakati wa ukaguzi wa migodi.
Wakati huohuo, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Simiyu, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa (RMOs), Maige Makolobela, alieleza kuwa kikao hicho ni muhimu sana kwa wakaguzi kupata mafunzo ya pamoja, kubadilishana uzoefu, na kujifunza kutoka kwa wenzao wanaosimamia migodi mikubwa. Aliongeza kuwa kuna vijana wengi wamejiunga na Tume ya Madini hivi karibuni, na vikao kama hivi ni fursa nzuri kwao kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu sekta hiyo. "Tuna vijana wameingia Tume ya Madini bado hawajafahamu vitu vingi, hivyo ni fursa nzuri kwa vijana katika sekta yetu kujifunza kupitia vikao kazi kama hivi," alisema Makolobela. Alisisitiza kuwa Sheria ya Baruti ni ya zamani, na maboresho yanahitajika ili kuendana na ongezeko la shughuli za migodi nchini.