Katika Joto la kampeni za kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu, mgombea ubunge wa Jimbo la Kinondoni kupitia tiketi ya chama cha CHAUMMA, Bi. Moza Ally, ameweka bayana mkakati wake kabambe wa kuwawezesha kiuchumi wananchi endapo atapata ridhaa ya kuongoza. Akihutubia umati wa wakazi waliojitokeza katika Uwanja wa Sumaye uliopo Kata ya Kigogo, Moza ameahidi kuleta mapinduzi katika usimamizi wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri.
Moza amewahakikishia wananchi wa Kinondoni, hasa makundi ya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu, kwamba ndani ya siku 100 za kwanza ofisini kwake, atahakikisha mfumo mzima wa utoaji mikopo hiyo unabadilishwa na kuwa wa wazi na wa haki. Alisema changamoto kubwa inayokabili mpango huu muhimu wa serikali ni urasimu na upendeleo, mambo ambayo ameahidi kuyatokomeza kabisa.
"Sitakubali kuona fursa hizi zinapotea au zinawanufaisha wachache kwa misingi ya undugu au itikadi za kisiasa. Nitakuwa mbunge wa watu wote," alisisitiza Bi. Moza huku akishangiliwa.
Ili kutimiza azma yake, ameeleza kuwa atazindua mpango maalum wa kutembea nyumba kwa nyumba ili kuorodhesha wajasiriamali wote wenye nia ya kunufaika na mikopo hiyo. Aidha, alitangaza kuwa ofisi yake itakuwa na mwanasheria atakayetoa msaada wa kisheria bila malipo kwa vikundi vyote, ili kuwawezesha kukidhi vigezo na masharti ya kisheria ya kupata mikopo hiyo. Alisema hatua hii itapunguza gharama na kuondoa vikwazo vinavyowakatisha tamaa wengi.
Akijinasibu kuwa "Mbunge wa watu" na si "mbunge wa mfukoni," Moza aliahidi kuwa milango ya ofisi yake itakuwa wazi kwa kila mwananchi bila kuhitaji kutoa fedha ili kumuona. Alisema, "Nipeni imani yenu, nami nitawatumikia kwa uadilifu mkubwa na kuhakikisha sauti ya Kinondoni inasikika."
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CHAUMMA Mkoa wa Dar es Salaam, Ndugu Henry Kileo, aliyekuwa ameambatana na mgombea huyo, aliwasihi wakazi wa Kinondoni kujitokeza kwa wingi Oktoba 29 ili kuwachagua viongozi wenye dira ya maendeleo, huku akitaja mojawapo ya sera za chama chao kuwa ni kuboresha lishe kwa wanafunzi mashuleni.