ZITTO KABWE Atikisa KIGOMA: Ahadi ya Barabara za Lami, Bima ya Afya Kwa Wote na Bilioni 1 kwa Wajasiriamali

politics | Tue Oct 28 2025


ZITTO KABWE Atikisa KIGOMA: Ahadi ya Barabara za Lami, Bima ya Afya Kwa Wote na Bilioni 1 kwa Wajasiriamali

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kigoma Mjini kupitia tiketi ya Chama cha ACT Wazalendo, Ndugu Zitto Kabwe, amehitimisha kampeni zake leo, Oktoba 28, 2025, kwa kutoa ahadi za kijasiri za kutetea maslahi na haki za wananchi wa Kigoma endapo atarejeshwa Bungeni.


Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na maelfu ya wafuasi wake, Zitto alisisitiza kuwa kipaumbele chake cha kwanza kitakuwa ni kuboresha miundombinu ya barabara. Ameahidi kukomesha kero ya vumbi na makorongo kwa kuhakikisha barabara zote muhimu katika kata mbalimbali za mji huo zinajengwa kwa kiwango cha lami.


"Tutajenga mji ambao hauna makorongo. Tutajenga barabara zinazopitika. Mambo hayo nitayakomesha," alisema Zitto, akiongeza kuwa kazi ya kuendeleza mji huo itakuwa rahisi kwani tayari wametengeneza mpango kabambe wa maendeleo wa miaka 20 kipindi walipokuwa wakiongoza Manispaa ya Kigoma-Ujiji.


Afya Kipaumbele: Bima kwa Wote


Katika sekta ya afya, Zitto alieleza kuwa ameguswa na changamoto za kiafya zinazowakabili wananchi kutokana na umasikini. Aliahidi kuanzisha mfuko wa hifadhi ya jamii utakaowezesha kila mkazi wa Kigoma kupata huduma za matibabu bila ubaguzi. "Ninaomba mnipe nafasi nikaangaike na afya zenu, kuhakikisha kila mtu anapata bima ya afya," alisema.


Aidha, aliahidi kuwa atahakikisha hakuna mwanamke yeyote atalazimika kulipa fedha yoyote anapokwenda kujifungua, akisisitiza kwamba ahadi hizi zinawezekana endapo kutakuwepo na dhamira ya kweli ya kisera na uongozi wenye kujali.


Mtaji kwa Wajasiriamali na Dira ya Biashara


Kama njia ya kuinua uchumi, Zitto amerejea ahadi yake ya kutoa Shilingi Bilioni Moja (Sh. 1 Bilioni) kama mikopo nafuu kwa wafanyabiashara wadogo na wajasiriamali. Mikopo hii inalenga kuwaepusha wafanyabiashara na masharti magumu yanayotolewa na taasisi za kifedha.


Akizungumzia dira yake ya kiuchumi kwa Kigoma, Zitto anataka kuifanya Kigoma kuwa kituo kikuu cha biashara cha kanda ya Afrika Mashariki. Alisema ujenzi wa Bandari ya Ujiji ni muhimu kwani mji uko kimkakati kwenye jiografia ya nchi za Maziwa Makuu. Ndoto yake ni kuona wafanyabiashara kutoka nchi jirani kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Burundi wakinunua bidhaa Kigoma badala ya kwenda Kariakoo, Dar es Salaam.


Kwa upande wa elimu, Zitto ameahidi kupigania ongezeko la shule za sekondari za kidato cha tano na sita ili kuongeza fursa za elimu kwa vijana. Pia, ameahidi kuendelea kutetea haki za wananchi, ikiwemo kuhakikisha raia wote wanapatiwa vitambulisho vya Taifa (NIDA) bila ubaguzi.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.