Moza wa Chauma Atikisa Kinondoni: Aahidi Kufuta Michango Shuleni, Kodi za Pedi na Bili za Maiti Hospitalini

politics | Wed Sep 24 2025


Moza wa Chauma Atikisa Kinondoni: Aahidi Kufuta Michango Shuleni, Kodi za Pedi na Bili za Maiti Hospitalini

Chama cha Ukombozi wa Umma (Chauma) kimewataka wakazi wa Jimbo la Kinondoni kuitumia siku ya Oktoba 29 kama "siku ya ukombozi" kwa kumchagua mgombea wake wa ubunge, Moza Ally. Katika mkutano wa kampeni uliofanyika leo, chama hicho kilimnadi Moza kama sauti halisi ya wananchi, huku mgombea huyo akitoa ahadi nzito zinazogusa moja kwa moja maisha ya kila siku ya wapiga kura.


Akihutubia umati, Moza Ally alisema akipata ridhaa ya kuwa mbunge, atahakikisha anapambana na kero sugu zinazowatesa wananchi. Alianza na sekta ya elimu, akipinga vikali kile alichokiita unafiki wa "elimu bure" huku wazazi wakiendelea kushurutishwa kutoa michango mbalimbali. "Niazimieni imani yenu, nikiingia bungeni hakuna mzazi atakayedaiwa tena michango ya shuruti kama hizo elfu mbili mbili. Tatizo likitokea, ofisi ya mbunge itakuwa wazi kwa ajili yenu," aliahidi Moza. Aliongeza kuwa atahakikisha shule zinapata walimu wa kutosha ili kuondoa utaratibu wa wazazi kulipia walimu wa ziada.


Moza pia alionesha dhamira ya kuwatetea wasichana na wanawake. Aliahidi kulipeleka bungeni suala la hedhi salama, akisema atapambana kuhakikisha kodi zote kwenye taulo za kike (pedi) zinaondolewa ili kila mzazi aweze kumudu gharama za kumnunulia binti yake. Katika sekta ya afya, aliahidi kuwa huduma za kujifungua kwa akina mama hospitalini zitakuwa bure kabisa.


Akitumia msemo "aliyeshiba hamjui mwenye njaa," Moza alisema yeye anayatambua machungu ya wananchi wenzake. Aligusia suala la familia kufiwa na ndugu lakini zikakwama kumchukua marehemu kwa ajili ya mazishi kutokana na madai ya bili za matibabu. "Jambo hili la kudai bili za maiti litabaki kuwa historia Kinondoni. Ni unyama kumzuia marehemu asizikwe kwa heshima," alisisitiza.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chauma Mkoa wa Dar es Salaam, Henry Kileo, alisema Moza ni kiongozi sahihi atakayepigania kuondolewa kwa sheria kandamizi. Naye mgombea udiwani wa Kata ya Tandale, Rahim Derenya, aliahidi kutatua kero ya maji na kuhakikisha wakazi wanafungiwa mita za maji za malipo ya kabla, sawa na mfumo wa LUKU za umeme.

I recommend this article.

You can participate in article recommendations up to 50 times within 24 hours.


0 comments


Messages unrelated about this certain topic may be deleted or restricted.

0/300
Loading...

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.