Rais Samia Suluhu Hassan ametoa msimamo wake kuhusu usawa wa kijinsia, akieleza kuwa ingawa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuhakikisha usawa, kuna baadhi ya majukumu ya asili kati ya wanaume na wanawake ambayo hayawezi kubadilishwa na harakati za usawa.
Akizungumza kwa hisia kali jijini Arusha katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Rais Samia alisisitiza kuwa harakati za kutetea usawa wa kijinsia zinapaswa kuelekezwa kwenye maeneo yanayohitaji mabadiliko, lakini si katika majukumu ya asili ya uumbaji. "Kuna mambo ambayo mpaka dunia itakwisha, wanawake na wanaume hatutakuwa sawa. Mimi kama mwanamke, Mungu amenipa kazi ya kubeba mtoto tumboni mwangu na kumleta duniani, kazi ambayo mwanaume hataweza kuifanya hata siku moja, hata maendeleo gani yafanyike," alisema Rais Samia kwa msisitizo.
Aliongeza kuwa, kwa upande mwingine, wanaume wamepewa jukumu la kuweka mbegu ili mwanamke apate ujauzito na kulea mtoto, jukumu ambalo mwanamke hawezi kulifanya. "Hapo hakuna cha usawa, tunaendelea kama Mungu alivyotuumba," alisisitiza.
Licha ya changamoto zilizokuwepo hapo awali, Rais Samia alibainisha kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuongeza ushiriki wa wanawake katika maamuzi ya kitaifa. "Hali ilivyokuwa huko nyuma katika taasisi za kufanya maamuzi haikuwa ikiridhisha, lakini sasa ni tofauti. Tunaona asilimia ya wabunge wa kike haipungui 33%. Pia, katika nafasi za udiwani kuna idadi inayotakiwa kisheria, na hata kwenye baraza la mawaziri tunajitahidi kuhakikisha wanawake wanapewa nafasi," alisema.
Kauli ya Rais Samia inaonyesha dhamira ya serikali katika kuhakikisha kuwa wanawake wanashiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa, huku akisisitiza umuhimu wa kutambua tofauti za kiasili kati ya jinsia. Mjadala wa usawa wa kijinsia unaendelea kuvuta hisia miongoni mwa Watanzania, huku wengi wakikubaliana na Rais Samia kuwa kuna maeneo yanayohitaji usawa, lakini pia kuna majukumu ya asili ambayo hayawezi kubadilishwa. Hii inaleta mjadala mpana katika jamii kuhusu mipaka ya usawa na jinsi ya kuheshimu majukumu ya asili huku tukiendelea kupigania usawa katika maeneo mengine.