Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amewataka wanawake nchini kuwa wabunifu na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya taifa. Akizungumza jijini Dar es Salaam kwenye mahafali ya 10 ya Programu ya Mwanamke Kiongozi, aliwapongeza wahitimu 110 na kuwataka kutumia ujuzi walioupata kwa manufaa ya jamii nzima.
Rais Samia aliwahimiza wahitimu hao kuwa mstari wa mbele kufungua njia kwa wengine, si wanawake pekee bali pia wanaume, ili kuleta usawa wa kijinsia na maendeleo jumuishi. Alipinga vikali dhana potofu kwamba mwanamke ana nafasi ndogo katika jamii, akisisitiza kuwa wanawake wana uwezo sawa na wanaume katika uongozi na sekta mbalimbali.
Akigusia suala la siasa, Rais Samia alisisitiza umuhimu wa ushiriki wa wanawake, hasa katika kipindi hiki ambacho taifa linaelekea kwenye uchaguzi mkuu. "Ni muhimu wanawake kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi sawa na wanaume. Pia, hakikisheni mnaandikishwa kwenye daftari la wapiga kura ili muweze kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi," alisema Rais Samia.
Hafla hiyo ilifanyika sambamba na Mkutano Mkuu wa Saba wa Mwaka, ambao ulikuwa na lengo la kuwawezesha wanawake na wasichana kushiriki katika uongozi. Mkutano huo uliandaliwa chini ya kaulimbiu "Haki, Usawa na Uwezeshwaji," ikilenga kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika nyanja zote za maendeleo.
Rais Samia alieleza kuwa serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wanawake kushiriki katika uongozi na maendeleo ya kiuchumi. Alitoa mfano wa programu mbalimbali za uwezeshaji wanawake ambazo serikali imezianzisha ili kuwapa wanawake ujuzi na mitaji ya kuanzisha biashara.