Macho na masikio ya wafuatiliaji wengi wa siasa na sheria nchini Tanzania yanaelekezwa katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, ambapo leo Jumanne, Oktoba 14, 2025, hatima ya mvutano mkali wa kisheria katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, inatarajiwa kujulikana. Jopo la majaji watatu linatazamiwa kutoa uamuzi mdogo ambao utaweka mwelekeo wa namna kesi hiyo itaendelea.
Uamuzi huo unaosubiriwa kwa hamu unatokana na malumbano makali yaliyoibuka mahakamani Ijumaa iliyopita. Kiini cha mzozo ni ombi la Tundu Lissu, ambaye anajiwakilisha mwenyewe, la kutaka maelezo aliyoyatoa shahidi wa pili wa upande wa mashtaka, Mkaguzi wa Polisi John Kaaya, yapokewe na mahakama kama kielelezo cha upande wa utetezi. Lissu anashikilia kuwa maelezo hayo yana mkinzano na ushahidi ambao shahidi huyo anautoa sasa mahakamani, hivyo ni muhimu kwa mahakama kuyapokea ili kupima uaminifu wa shahidi.
Hata hivyo, upande wa Jamhuri, ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Ajuaye Zegeli, ulipinga vikali ombi hilo. Zegeli alidai kuwa Lissu hakufuata taratibu sahihi za kisheria katika kuwasilisha ombi hilo. Alisema lengo la kutumia maelezo ya awali ya shahidi si kuyafanya kielelezo, bali ni kumkabili na kumuonyesha maeneo anayojichanganya. "Mshtakiwa ameshindwa kumdodosa shahidi kuhusu maeneo hayo yenye utata kabla ya kuomba yapokewe. Anachotakiwa kufanya ni kumuuliza shahidi, siyo kuiomba mahakama iyapokee yenyewe," alisisitiza Zegeli, akiungwa mkono na Wakili Mkuu Ignas Mwinuka.
Akijibu mapigo, Lissu aliishutumu serikali kwa kutaka "kula keki na kubaki nayo," akisema anafuata miongozo iliyowekwa na Mahakama ya Rufani katika kesi za nyuma. Alitaja kesi za kihistoria kama za Lilian Jesus Fotes na Shadrack Sospiter, ambazo ziliweka bayana utaratibu wa kwanza kumsomea shahidi maelezo yake, kumuonyesha kinachokinzana, na kisha kuiomba mahakama iyapokee kama kielelezo. "Waheshimiwa majaji, sheria ziko wazi hapa nchini, msikubali kupelekwa India. Pingamizi hili halina msingi," alijenga hoja Lissu.
Kufuatia hoja hizo nzito, jopo la majaji linaloongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, likisaidiana na Majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde, litaamua leo iwapo maelezo hayo ya Mkaguzi Kaaya yatakubaliwa kama kielelezo. Uamuzi huu utafungua njia kwa Lissu kuendelea kumhoji maswali ya kina shahidi huyo, ambaye anatoka kitengo cha doria mtandaoni cha Jeshi la Polisi.
Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini, akidaiwa kutoa maneno ya kichochezi Aprili 3, 2025, yenye lengo la kuhamasisha umma kuzuia na kuvuruga Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.